Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 02Article 555073

Habari Kuu of Thursday, 2 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Majibu ya serikali kuhusu kuunganisha NIDA na RITA

Majibu ya serikali kuhusu kuunganisha NIDA na RITA Majibu ya serikali kuhusu kuunganisha NIDA na RITA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema serikali haiwezi kuunganisha taasisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kutokana na tofauti za majukumu yake.

Majaliwa ameyasema hapo leo Septemba 2, 2021Bungeni akijibu swali la Abubakari Damian Asenga, mbunge wa Kilombero ambaye alishauri taasisi hizo ziunganishwe ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa ambavyo alisema kwa sasa vinacheleweshwa sana.

“NIDA inatoa kitambulisho cha Taifa ambacho kinamtambulisha Mtanzania na hakitolewi kwa mtu ambaye si raia wakati RITA inatoa cheti cha kuzaliwa kikionesha kuwa umezaliwa wapi, tarehe yako ya kuzaliwa na pia wanatoa cheti cha kifo.”

Amesema RITA inaweza kutoa cheti cha kuzaliwa kwa mtu yeyote aliyezaliwa Tanzania kwa sababu pale hospitalini akishazaliwa mtoto, taarifa zitaonesha hivyo na inaweza kutoa cheti kwa huyo mtoto hata kama siyo Mtanzania.

“Mtu anaweza kuzaliwa Tanzania na kupewa cheti cha kuzaliwa kwa kuwa amezaliwa ndani ya nchi yetu, lakini mtu huyo anaweza asiwe Mtanzania kwa mujibu wa sheria zetu.”

Amesema taasisi hizo zinaweza kupeana taarifa pale inapobidi lakini vyote vina majukumu tofauti.

“Urasimu unaosemwa hapa nimeusikia wakati nilipofanya ziara kwenye mikoa ya pembezoni. Na huko nimekuwa nikisisitiza umakini katika kuchunguza taarifa za waombaji.”

“Kuchelewa kwetu kwenye mikoa ya pembezoni ambako pia kunaitwa urasimu, kunafanywa kwa nia nzuri ili kujiridhisha kama kweli anayeomba kitambulisho ni raia wa Tanzania,” amesisitiza.

Nataka niwahakikishie Watanzania kwamba mtu yeyote Mtanzania ambaye Baba na Mama ni Watanzania, ni lazima atapata kitambulisho cha Taifa, kikubwa wawe na subira. Nasi kwa upande wetu tumejitahidi kuongeza vifaa na watumishi ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo hasa kwa wale ambao wamehakikiwa na wanastahili.”