Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542182

Habari Kuu of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Majina JKT awamu ya pili yatangazwa

Majina JKT awamu ya pili yatangazwa Majina JKT awamu ya pili yatangazwa

JESHI la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza awamu ya pili ya majina ya vijana watakaopata mafunzo hayo huku likitaka vijana wote walioitwa kuhudhuria mafunzo hayo na hawajaripoti, kufanya hivyo ifikapo Juni 17, mwaka huu.

Aidha, JKT limesema mafunzo kwa vijana wanaojiunga nalo kwa mujibu wa sheria yatakuwa ya miezi mitatu na si mwaka mmoja.

Kaimu Mkuu wa Utawala wa JKT, Kanali Hassan Mabena, alisema mafunzo hayo yatafanyika kwa miezi mitatu ili kutoa nafasi kwa vijana kujiunga na vyuo vikuu ifikapo Septemba.

“Kumekuwepo na dhana mitaani kuwa mafunzo ya mujibu wa sheria yanatolewa kwa mwaka mmoja, jambao ambalo limefanya baadhi ya vijana kutoripoti kwenye makambi waliyopangiwa, usahihi ni kuwa mafunzo yanatolewa kwa miezi mitatu,” alisema.

Hata hivyo alisema, mchakato wa kuongeza muda wa mafunzo kuwa mwaka mmoja unaendelea.

“Tunaendelea na mchakato wa kuyafanya mafunzo haya kwa mujibu wa sheria, kuwa mwaka mmoja; hii ina maana itahusisha pia kubadilika kwa mihula ya masomo na muda wa kujiunga na vyuo.”

“Kwa sasa tuko katika hatua za kuandaa andiko litakalopelekwa kwenye Baraza la Mawaziri ili lijadiliwe, hivyo mafunzo kutolewa kwa mwaka mmoja huenda yakaanza mwaka ujao endapo taratibu zote zitakamilika.”

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Brigedia Jenerali Rajabu Mabele, Kanali Mabena alisema jeshi limetoa nyongeza ya majina ya vijana waliohitimu Kidato cha Sita Mwaka 2021 kwenda kuungana na vijana wenzao walioitwa awali kuhudhuria mafunzo hayo.

Alisema vijana wote walioitwa kuhudhuria mafunzo ya JKT na hawajaripoti, wanapaswa kuripoti haraka katika kambi walizopangiwa.

“Mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria mwaka 2021 yataendeshwa kwa muda wa miezi mitatu tu, vijana hao walioitwa katika orodha ya pili na ambao hawajaripoti hadi sasa, wanatakiwa kuripoti katika makambi ya JKT waliyopangiwa mara moja na mwisho wa kuripoti ni Juni17 mwaka huu,” alisema.

Aliwataka wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho kuripoti katika kambi ya JKT YA Ruvu iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.

“Mkuu wa JKT Brigedia Jenerali Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote walioitwa ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kukijenga na kulitumikia taifa letu,” alisema Mabena.

Join our Newsletter