Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 21Article 558811

Siasa of Tuesday, 21 September 2021

Chanzo: mwananchidigital

Makada CCM waamka na kauli ya Rais Samia 'mgombea mwanamke'

Makada CCM waamka na kauli ya Rais Samia Makada CCM waamka na kauli ya Rais Samia

Hoja ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwataka wanawake kusimamisha Rais mwanamke katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, imefichua mambo yaliyojificha ndani ya CCM kwa baadhi ya makada kuanza kutengeneza safu kwa ajili ya kupanga mitandao ya uchaguzi mkuu huo.

Taarifa zilizokusanywa zikiwanukuu baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), wabunge wa CCM na makada wengine, zinaonyesha uchaguzi ndani ya CCM mwakani utakuwa ni ‘vita’ kubwa.

Vyanzo ndani ya CCM vinadai yapo makundi ya makada wanaopanga safu za watakaogombea nafasi mbalimbali ndani ya chama ili baadaye wawe kama mtaji wa kuwatafutia kura watakaogombea 2025.

Hata hivyo, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga alisema kwa sasa hawajapata taarifa ila wakibainika watashughulikiwa.

Septemba 15, Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM alitoa kauli hiyo katika maadhimisho ya Siku ya Demokrasia Duniani na kusema Rais aliyepo sasa hivi aliwekwa kwa kudra za Mwenyezi Mungu hivyo kuwataka kusimamisha mwanamke mwaka 2025.

“Nataka niwaambie wanawake bado hatujaweka Rais mwanamke. Rais huyu amekaa kwa sababu ya kudra ya Mungu na matakwa ya Katiba.

“Tulichokichangia sisi na mama zetu na dada zetu akina Anna Abdalah ni kusukuma mpaka mwanamke akawa Makamu wa Rais. Ule ndio mchango mkubwa tumeufanya wanawake,” alisema Rais.

Kauli hiyo ya Rais ni kama imefungua milango ya watia nia kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani kuanza kujipanga kimyakimya kwa kuanzia kwenye uchaguzi ndani ya CCM mwaka 2022 kupanga safu zao.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, wanaopanga safu wanaona ule utamaduni wa kumwachia Rais anayetokana na CCM kuongoza vipindi viwili haingii kwa Rais Samia, kwani hakuingia kupitia sanduku la kura.

Mjumbe mmoja wa NEC ya CCM alilidokeza gazeti hili kuwa kuna fukuto kubwa ndani ya CCM na uchaguzi wa ndani wa chama unataka kutumiwa na baadhi ya makada kupanga safu za uongozi lakini lengo ni kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Hili linaendelea karibu nchi nzima na linafanyika kwa siri kwa sababu taratibu za chama haziruhusu. Kwa jicho la kawaida utadhani wanatafuta uongozi ndani ya CCM lakini ni harakati za kuelekea mwaka 2025,” kilidokeza chanzo chetu.

Mkoani Kilimanjaro mathalan, baadhi ya makada wanaojipanga kugombea ubunge wanadaiwa kufanya vikao vya siri na baadhi ya viongozi wa CCM wa matawi na kata wa sasa ili kupanga safu ya watakaogombea mwakani.

“Hili linawasumbua sana wabunge walioko madarakani na kuwavuruga maana wanashindwa ku-concentrate (kujikita) katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi. Wao wanaona watakaowavusha mwaka 2025 ni hawa watakaochaguliwa mwakani,” alidai mbunge mmoja aliyeomba asitajwe jina.

Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Patrick Boisafi alipoulizwa juu ya uwepo wa makada walioanza harakati za kuutumia uchaguzi wa ndani wa CCM mwakani kupanga safu kwa ajili ya mwaka 2025 alisema naye amezipata taarifa hizo.

“Nakisikia kwa mbali, lakini watu hao hawajajitokeza kwetu kwa sababu chama bado hakijatoa taratibu za uchaguzi wa mwaka 2022 lakini kuna watu wanajitengeneza tu kubebana.Wanatengeneza safu ndani ya chama lakini kama unavyosema intention (dhamira) yao sio kugombea ndani ya CCM mwaka 2022, bali wanajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2025. Tukiwabaini tutawachukulia hatua,” alisisitiza.

Uwepo wa wanasiasa wanaojipanga kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 iliwahi kudokezwa na Rais Samia Aprili mwaka huu wakati akiwaapisha mawaziri aliokuwa amewateua na kuwaonya kuhusu harakati hizo za mapema.

“Nafahamu 2025 iko karibu na kawaida yetu sijui kama Watanzania ama kote ulimwenguni inapoingia kipindi cha pili cha rais aliyepo watu kidogo mnakuwa na lile na hili kuelekea mbele. Nataka kuwaambia acheni,” alisema.

Rais Samia alisema si jambo la busara wanasiasa kuanzisha kampeni za mapema kwani kwa kufanya hivyo kutahujumu juhudi za Serikali ya kutoa huduma na kuwaambia rekodi yao ndio itawafuata katika maisha.

Rais Samia kuwakumbusha wanasiasa walio na nia ya kuwania nafasi mbalimbali kwamba rekodi yao ya utendaji kazi katika kuwahudumia Watanzania itawafuata katika maisha yao yote.