Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572647

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: IPPmedia

Makali mgawo wa maji yazidi kung’ata

Makali mgawo wa maji yazidi kung’ata Makali mgawo wa maji yazidi kung’ata

Makali ya mgawo wa maji jijini Dar es Salaam, yameshika kasi huku baadhi ya maeneo wakikosa huduma hiyo kwa zaidi ya wiki moja ba bei ya galoni moja la lita 20 imefika hadi Tsh.1,500.

Aidha, katika baadhi ya maeneo, hakuna maji kwa takribaki siku tano hali inayowalazimu wengi kutumia maji ya visima ambayo nayo yamepanda bei kufikia Sh. 500.

Kutokana na hali hiyo, Waziri wa Maji, Juma Aweso, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kugawa maji kwa usawa.

Hivi karibuni, ratiba ya mgawo wa maji iliyotolewa na DAWASA kwa maeneo tofauti ilionyesha kuwa maji yatatoka kwa wiki siku za Jumanne, Alhamisi, Jumamosi na Jumapili kwa muda wa saa 10 kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 1:00 jioni.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mosi Joshua, mkazi wa Tabata Bima, alibainisha kuwa katika eneo hilo maji hutoka mara mbili kwa wiki na kwa saa chache kinyume cha ratiba ya DAWASA.

Joshua alisema hali hiyo imesababisha uhitaji wa maji kuwa mkubwa huku bei zikizidi kupaa kutoka Sh. 200 hadi 1,000 na maeneo mengine Sh. 1,500 kwa dumu lenye ujazo wa lita 20.

“Upatikanaji wa maji umekuwa ni changamoto kubwa katika eneo hili kila mtu analalamika maji. Kwenye ratiba ya mgawo walionyesha siku yakitoka yanakaa saa 10, lakini imekuwa tofauti kwani siku zingine yanatoka ndani ya saa moja yanakatika.

“Hiyo inasababisha uhaba wa maji kuzidi kuwa mkubwa kwani hata yakitoka yanakuwa machache ukilinganisha na mahitaji. Unaishia kuchota ndoo mbili, hizo zitumike kupikia, kuoga, kufulia watoto na matumizi mengine, kwa uhalisia wa kawaida ni jambo gumu,” alisema.

Maeneo mengine ni Mwenge kutokana na uhaba wa maji, bei ya galoni imeongezeka kutoka Sh. 300 hadi 1,000 kwa maji ya chumvi na Mbezi kutoka Sh. 250 hadi 500. Baadhi ya maeneo ya Salasala upatikanaji wa maji umekuwa mgumu kiasi cha baadhi ya maeneo kumaliza wiki moja bila huduma hiyo.

Pia baadhi ya maeneo yanatoka usiku wa manane ambao ni hatari kwa mtu kutoka kuteka maji huku wengine wakinunua kwa kati ya Sh.500 hadi 1,000 na wengine wanauza maji ya DAWASA.

Elihudi Shabani, mkazi wa Mbezi Juu, alisema kwa mujibu wa ratiba ya DAWASA maji yalipaswa yatoke mara moja kwa wiki kila Jumanne na alidai kuwa ni zaidi ya mwezi sasa hayajatoka.

Na uhaba wa maji ya bomba watu wengi wamekuwa wakitumia maji ya boza/chumvi ambayo awali yalikuwa yanauzwa Sh. 12,000 kwa tangi lenye ujazo wa lita 1,000 lakini gharama imepanda hadi Sh. 20,000 kutokana na uhitaji kuzidi kuwa mkubwa,” alisema Shabani.

WAZIRI AFUNGUKA

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza na uongozi wa DAWASA kuhusu mgawo wa maji, alisema mamlaka hiyo ihakikishe mfumo wa ugawaji unarejea kawaida.

“Niwasisitize watumishi wa mamlaka kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha mgawo wa maji unatolewa kwa uwiano bila upendeleo,” aliagiza Aweso.

Aliongeza kwa kuitaka DAWASA kutoa bei elekezi kwa watoa huduma binafsi wa maji kupitia magari (bowser), ili kuondoa sitofahamu iliyojitokeza kwa baadhi ya watu kuanza kuuza maji kwa bei zao wenyewe kwa kukiuka utaratibu uliowekwa na mamlaka husika.

Pia, Waziri Aweso aliahidi ushirikiano baina ya wizara na DAWASA katika kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kuhakikisha watu wote wanapata maji kwa wakati na mgawo kuwa na uwino sawa kila sehemu.

MBEYA WALALAMIKA

Jijini Mbeya baadhi ya maeneo wanalazimika kutumia maji ya visima kutokana na kukosekana kwa maji ya bomba na sasa wananunua kwa Sh. 500 ndoo ya lita 20.

Mkazi wa Manenane, Clinton Swilla, alisema upatikanaji wa maji ni changamoto kubwa hali inayowafanya kutokuwa na uhakika na bidhaa hiyo.

Naye Mkazi wa Lwambi, Angelica Sulusi, alisema ni wiki ya pili sasa hakuna maji na kuiomba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Mbeya kushughulikia kwa haraka tatizo na kuweka wazi kama kuna mgawo au la.

Katika taarifa yake kwa umma, Ofisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Neema Stanton, alisema sababu ya kukosekana kwa maji mara kwa mara ni kutokana na kukatika kwa umeme.