Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 16Article 542935

Habari za Mikoani of Wednesday, 16 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Makalla akerwa na uchafu, kupanga machinga

Makalla akerwa na uchafu, kupanga machinga Makalla akerwa na uchafu, kupanga machinga

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema hajaridhishwa na hali ya usafi mkoani humo hivyo atatoa mpango aliouandaa kwa kushirikiana na wataalamu unaoelekeza wafanyabiashara wadogo kupangwa vipi kila wilaya.

Makalla alisema hayo jana alipozungumza na watendaji pamoja na madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake inayoendelea mkoani humo.

Alisema hajaridhishwa na hali ya usafi katika Mkoa wa Dar es Salaam ambao ni lango la biashara, uso wa nchi, mkoa mkubwa wenye bandari pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa.

“Dar es Salaam kwa sasa haipo katika usafi, nilitoka kumpokea mgeni hivi karibuni Rais wa Botswana kuanzia Airport(Uwanja wa Ndege) mpaka Mnazimmoja kuna vibanda, takataka, moshi wa gesi, moshi wa kuni ni aibu.

“Kosa si la wale wanaofanya ile biashara ila sisi tulisahau wajibu wetu wa kuwaweka vizuri. Vibanda kila mahali. Hakuna mahali utapita vizuri. Nje ya Shule ya Msingi Bunge vibanda, IFM (Chuo cha Usimamizi wa Fedha) vibanda, nenda daraja la Kijazi watu wanauza supu, miwa, vitunguu. Ni shaghalabaghala,” alisema.

Alisema kiongozi anapaswa kutambua tatizo na kurekebisha. Kama kiongozi akijua tatizo asipotatua huyo ni tatizo.

“Lazima tuiweke Dar iwe safi, nendeni nchi zozote utaratibu upo. Hapa fanya hiki hapa usifanye. Sasa Dar tumeruhusu kila mtu afanye anachotaka. Lazima tujenge heshima ya mji huu, ni uso unapokea watu mbalimbali. Nitaleta mpango wangu mzuri, nimeandika na kushirikisha wataalamu namna ya kuweka mkoa huu safi na kuupanga vizuri wafanye biashara,” alisema Makalla.

Alisema hali imefikia hapo kwa kuwa kuna mahali viongozi walibaki bila kutoa mwongozo. Alisema mpango huo atakaouleta utaonesha athari zilizopo kiusalama na kijamii endapo Dar es Salaam isipopangwa vizuri.

Alizungumzia usalama katika mkoa huo kuwa ni shwari hivyo itawafanya wananchi kufanya biashara zao kwa utulivu. Ameagiza wakuu wa wilaya kuwa ajenda ya ulinzi na usalama iwe ya kudumu kuanzia kwenye mtaa, kata na wilaya.

“Naamini tukisimamia hili tutatoa nafasi kwa wananchi kuendelea na uzalishaji mali ili wajipatie kipato,” alisema.

Aliwataka pia viongozi wa manispaa hiyo kujielekeza katika kutatua kero ya wananchi.

“Falsafa yangu palipo na kero ya wananchi mimi nipo. Tuwapokee watu vizuri na kutenga siku ya kusikiliza kero zao,” alisema.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Abdallah Mtinika alisema Temeke inakwenda vizuri na timu ya menejimenti, hivyo watakuwa wa kwanza kuonesha mfano.

Mkuu wa Wilaya Temeke, Godwin Gondwe alisema katika wilaya hiyo kuna watoto wengi wanaoingia darasa la kwanza hivyo wamejenga madarasa 134 kwa awamu na yako kwenye hatua nzuri