Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 27Article 559780

Habari Kuu of Monday, 27 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Makamba autwisha mzigo uongozi mpya Tanesco

Makamba autwisha mzigo uongozi mpya Tanesco Makamba autwisha mzigo uongozi mpya Tanesco

WAZIRI wa Nishati, January Makamba ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lijiendeshe kisasa, liongeze ufanisi na limalize changamoto zinazowakabili wananchi.

January alitoa maagizo hayo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na viongozi wakuu wa Tanesco, bodi mpya ya shirika hilo na mameneja wa mikoa na kanda

Alisema anataka kuona Tanesco inakuwa bora nchini na barani Afrika na shirika hilo liongeze ufanisi ili liuze umeme nje ya nchi.

January alisema wananchi wana malalamiko kuhusu huduma za shirika hilo ikiwamo kero ya kukatika umeme na kuiagiza menejimenti ishirikiane na bodi kutafuta dawa ya tatizo hilo na baadaye bei ya umeme ipungue.

"Tanesco hii yenye muelekeo mpya inapaswa kuja na majibu ya kero za watumiaji wa umeme, binafsi sitapenda kusikia napigiwa simu kuwa umeme umekatika sehemu fulani, tukidhibiti haya tutafika mbali," alisema.

Jauary alisema anataka kuona mabadiliko ya uongozi Tanesco yanakuwa chachu ya mageuzi ili baada ya miaka michache shirika hilo liwe na heshima na thamani kubwa nchini na Afrika.

"Hakuna sababu yoyote kwa shirika hili kubwa kusuasua, jambo la msingi ni weledi wa kila mmoja ili tuweze kufika tunapotaka," alisema.

January alisema yamefanyika mabadiliko ya uongozi kwenye shirika hilo ikiwamo nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji na bodi ili kuongeza ufanisi na heshima.

"Shirika lilikuwa likijiendesha kwa njia zisizo na ufanisi, shirika kama Tanesco halipaswi kwenda mzobe mzobe, leo ni kama linazaliwa upya na kila mmoja atekeleze majukumu yake ipasavyo ili tuweze kulifikisha mbali," alisema.

Alisema serikali itahakikisha Tanesco haiingiliwi na mambo ya kisiasa na ndiyo maana hata uteuzi wa nafasi za uongozi ulizingatia watu wenye sifa.

Aliwataka wateule wapya wasimamie na kuzingatia suala la rasilimali ndani ya shirika kwa kusimamia masuala ya maslahi ya watumishi ukiwamo upandishaji vyeo kwa ajili ya kuwajengea morali ya kufanya kazi.

Mkurugenzi Mtendaji Tanesco, Maharage Chande alisema malengo yake ni kuona shirika hilo linakuwa na ufanisi wa kiutendaji na kutoa matokeo yenye tija kwa taifa.

Alisema anaamini kama watendaji na watumishi wote waliopo ndani ya shirika hilo watashirikiana na kutimiza ipasavyo majukumu yao, dhima na malengo ya kuifanya Tanesco kuwa ya kisasa na mwelekeo mpya wenye faida kwa taifa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Omary Issa aliahidi kuwa bodi hiyo itafanya kazi kwa kuzingatia taratibu na akataka kila mtu awajibike katika nafasi yake.

Alisema bodi hiyo itatekeleza majukumu yake bila ya kuliingilia shirika hilo ili watendaji wawaeze kuboresha utendaji.