Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 09Article 584404

Siasa of Sunday, 9 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Makamu wa Rais achukua fomu ACT-Wazalendo

Makamu wa Rais achukua fomu ACT-Wazalendo Makamu wa Rais achukua fomu ACT-Wazalendo

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo katika uchaguzi wa chama unaotarajiwa kufanyika Januari 29, mwaka huu.

Othman ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, alikabidhiwa fomu hiyo na Naibu Mkurugenzi wa kampeni za chama hicho, Muhene Said Rashid katika makao makuu ya chama Vuga, baada ya kukidhi vigezo vyote ikiwemo kukaguliwa kwa kadi yake ya uanachama.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu ya kujaza kwa nafasi hiyo, Othman alisema amechukua fomu hiyo kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo awe daraja la kuunganisha chama na serikali.

Alisema amepewa heshima kubwa na chama na hajapata kuipata sehemu yoyote ya kupendekezwa kuwa makamu wa kwanza wa rais katika serikali ya umoja wa kitaifa na sasa ni wakati muafaka wa kufanya kazi kikamilifu katika chama na kuweza kufikia matarajio ya chama.

“Kwa ufupi nimechukua fomu kukidhi matarajio ya wanachama wa ACT-Wazalendo baada ya kunipendekeza kuwa makamu wa kwanza wa rais, sasa ni vizuri nichukue fomu kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama ili nitekeleze vizuri majukumu na maamuzi ya chama kikamilifu,” alisema.

Jumla ya wanachama watatu wa ACT-Wazalendo wamejitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi za juu za uongozi ikiwemo ya Mwenyekiti Taifa na Makamu mwenyekiti. Wanachama wengine waliochukua fomu kuwania nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho taifa ni aliyekuwa mwakilishi wa Jimbo la Ole pamoja na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Hamad Masoud.

Aidha, kiongozi mwandamizi wa chama hicho, Juma Duni Haji amechukua fomu kuwania nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho taifa baada ya kujiuzulu nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama mwishoni mwa mwaka jana, huku Sanani Masoud akichukua fomu kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Fatma Fereji, wanachama wote waliochukua fomu wanatakiwa kukamilisha mchakato wa kujaza fomu na kuzikabidhi ifikapo Januari 17, mwaka huu. Mkutano Mkuu wa taifa wa uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Januari 29, mwaka huu.