Uko hapa: NyumbaniInfos2020 09 25Article 510271

General News of Friday, 25 September 2020

Chanzo: HabariLeo

Mama Karume aelezea Mapinduzi na mwanamke

Mama Karume aelezea Mapinduzi na mwanamke

MJANE wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume, amesema Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, ndiyo yaliyofungua milango kwa kundi la wanawake kuwania nafasi za uongozi wa juu, kwani kabla ya hapo mwanamke hakuruhusiwa hata kupiga kura.

Mama Fatma alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Bumbwini, mkoa wa Kaskazini Unguja, katika mkutano wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye jimbo hilo.

“Alisema hadi mwaka 1960 hakuna mwanamke aliyeruhusiwa kushiriki katika mchakato wa uchaguzi kwa sababu mamlaka yote yalikuwa yakishikiliwa na utawala wa Kisultani kutoka Oman.”

''Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ndiyo yaliyofungua milango kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika ngazi za uongozi na kushika madaraka ya nafasi mbalimbali, pamoja na kupata elimu ya juu katika nchi mbalimbali marafiki za Ulaya,'' alisema.

Aliwataka wanawake kumchagua mgombea uwakilishi wa jimbo kupitia CCM, Mtumwa Peya Yussuf, ambaye amesema ameonesha uwezo mkubwa na ujasiri wa kuleta maendeleo, ikiwamo kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za wananchi.

Aliyataja baadhi ya mambo makubwa yaliyofanywa na mwakilishi huyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya uongozi wake kuwa ni pamoja na kuzipatia ufumbuzi changamoto za maji safi na salama katika shehia za jimbo hilo kwa kujenga visima na matanki ya maji.

''Nakumbuka alipoingia madarakani mwaka 2015 tulikuwa tunakabiliwa na changamoto ya maji safi na salama kwa baadhi ya shehia, amejenga visima na minara ya kuweka matangi ya maji na sasa wananchi wanafaidika na huduma hiyo kikamilifu,'' alisema.

Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni katika Jimbo la Bumbwini, Peya aliwaomba wananchi kumpa tena miaka mitano kwa ajili ya kukamilisha changamoto zilizobakia katika jimbo hilo. Alisema amejipanga kuona vikundi vya wajasiriamali vya akinamama na vijana vinaendelezwa kwa kupewa maarifa na kuibua miradi yenye tija.

“Awali shule zetu zilikuwa zinakabiliwa na tatizo la madawati na hivyo kuwafanya wanafunzi kusoma chini ya sakafu, sasa mambo yamebadilika na wanafunzi wanasoma katika mazingira ambayo yanatoa nafasi nzuri ya ufaulu,” alisema.

Akimnadi mgombea huyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Iddi Ame, alisema wamefanya tathmini na kubaini kwamba, wanawake wameonesha uwezo mkubwa wa kushika nafasi za uongozi na kuzifanyia kazi changamoto za wapiga kura.

''Nawaombeni wapigakura wa Jimbo la Bumbwini mchagueni mwanamke mwenzenu Mtumwa Peya, katika muda wa miaka mitano alifanya kazi kubwa kuona akinamama wanajifungua katika hospitali kubwa ya Bumbwini,'' alisema.

Join our Newsletter