Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 30Article 554383

Habari Kuu of Monday, 30 August 2021

Chanzo: ippmedia.com

Mambo matano yanatarajiwa kutikisa Bunge kesho Dodoma

Gwajima, tozo miamala ya simu kutikisa Bunge Gwajima, tozo miamala ya simu kutikisa Bunge

MKUTANO wa Nne wa Bunge la 12 unatarajiwa kuanza kesho jijini Dodoma huku tuhuma za kushusha hadhi na heshima zinazowakabili wabunge wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Askofu Josephat Gwajima na Jerry Silaa zikitarajiwa kuwa sehemu ya mambo yatakayotikisa.

Mbali na tuhuma dhidi ya wabunge hao wa Kawe na Ukonga, mtawalia, sakata la tozo za miamala ya simu linatarajiwa kuwa sehemu ya hoja zitakazoibuliwa wakati wa mijadala ya mkutano huo.

Vilevile, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitawasilisha taarifa zake kuhusu namna zilivyoshughulikia hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2019/20.

GWAJIMA, SILAA

Kwa siku tano mfululizo kuanzia Jumatatu ya wiki iliyopita, wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge waliketi kwa lengo la kuwahoji Askofu Gwajima na Silaa kutokana na tuhuma za kushusha hadhi na heshima ya Bunge zinazowakabili.

Kuhojiwa kwa wabunge hao ni maagizo ya Spika Job Ndugai, aliyeitaka kamati hiyo kuwaita na kuwahoji dhidi ya tuhuma hizo.

Wawili hao walihojiwa mbele ya kamati hiyo, mahojiano yakifanyika kwa siku mbili kwa kila shahidi. Awali kamati ilipanga kuwahoji kwa siku nne lakini ililazimika kuongeza siku moja kutokana na Silaa kushindwa kufika mbele ya kamati katika siku ya pili ya mahojiano.

Kama kamati ikiwakuta na hatia, itapendekeza adhabu dhidi yao ambayo itajadiliwa na Bunge ili ama kuridhiwa au kutoridhiwa. Kuna uwezekano taarifa ya kamati hiyo kuwasilishwa bungeni wakati wa mkutano huo utakaoanza kesho, lakini itategemea uamuzi wa uongozi wa Bunge.

TOZO ZA MIAMALA

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dodoma juzi, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alibainisha kuwa kesho serikali itaweka hadharani ilichokiamua kuhusu tozo za miamala ya simu baada ya kupokea ripoti ya kamati iliyoundwa kushughulikia suala hilo.

Suala hilo linatarajiwa kuwa sehemu ya hoja zitakazoibuliwa wakati wa mkutano huo wa Bunge, ikizingatiwa tayari Spika Ndugai ameshaweka wazi kuwa Bunge liko tayari kufanya marejeo ya sheria iliyoanzisha tozo hizo.

Huku serikali ikitangaza kukusanya Sh. bilioni 48 katika mwezi wa kwanza wa tozo hizo, wadau wamekuwa wakizipinga vikali kwa kile wanachodai kuongeza ugumu wa maisha kwa wananchi.

Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), Catherine Ruge, aliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki mkoani Dar es Salaam kuwa chama chao hakiungi mkono tozo hizo kwa kuwa zinaumiza wananchi hasa wanawake walioko vijijini ambao wanategemea kwa kiwango kikubwa kufanya miamala ya simu katika kuendesha shughuli zao za ujasiriamali.

HOJA ZA CAG

Wakati wa mkutano uliopita wa Bunge (Bunge la Bajeti), Spika Ndugai aliagiza PAC na LAAC kushughulikia hoja zilizoibuliwa na CAG katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2019/20 iliyowasilishwa bungeni Aprili mwaka huu.

Spika Ndugai aliagiza taarifa za kamati hizo ziwasilishwe wakati wa mkutano wa Septemba utakaoanza kesho badala ya mkutano wa Novemba ilivyokuwa imezoeleka awali.

Tayari kamati hizo zimeshawaita na kuwahoji watendaji wa taasisi na halmashauri zilizobainika kuwa na shida kwenye hesabu zake.

BIMA KWA WOTE

Juzi mjini Dodoma Msemaji Mkuu wa Serikali, Msigwa, aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari kuwa wakati wa mkutano ujao wa Bunge, serikali itawasilisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote na tayari Sh. bilioni 349 zimetengwa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa bima hiyo hata kabla ya kupitishwa kwa sheria yenyewe.