Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 25Article 573979

Habari Kuu of Thursday, 25 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Mambo matano yatakayodhibiti kupanda bei vifaa vya ujenzi nchini

Mambo matano yatakayodhibiti kupanda bei vifaa vya ujenzi nchini Mambo matano yatakayodhibiti kupanda bei vifaa vya ujenzi nchini

Baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu bei kubwa za vifaa vya ujenzi, hatimaye serikali imetaja hatua tano itakazochukua katika kukabiliana na kupanda kwa bidhaa hizo.

Moja kati ya hatua hizo ni pamoja na agizo kwa Tume ya Ushindani (FCC) kufanya uchunguzi na kuchukua hatua kisheria kwa waliopandisha bei ya saruji isivyo halali.

Aidha, imezuia usafirishaji wa shaba chakavu nje ya nchi ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za chuma nchini.

Hatua  nyingine ni kuiagiza FCC kuendelea kufuatilia mwenendo wa upandaji bei na kuwachukulia hatua stahiki wafanyabiashara wanaokiuka sheria ya ushindani, kupiga marufuku uuzaji nje ya nchi shaba chakavu.

Nyingine ni kurekebisha sheria na kanuni ili kuruhusu kuingizwa kwa urahisi zaidi malighafi zinazohitajika katika uzalishaji wa bidhaa za vyuma ikiwamo kuruhusu kuingizwa kwa vyuma chakavu kutoka nje kwa utaratibu utakaohakikisha inapatikana bila kuathiri mazingira ya nchi.

Pia katika mpango wa muda mrefu, serikali itatekeleza miradi kielelezo itakayowezesha kuzalisha chuma kingi nchini kwa ajili ya viwanda vya ndani na kuuza nje ya nchi.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, alibainisha hayo jana jijini hapa wakati akitoa tathmini ya mwenendo wa uzalishaji, usambazaji na bei za vifaa vya ujenzi kwa kipindi cha Septemba hadi Novemba, mwaka huu.

Amesema wizara hiyo imekuwa ikifanya tathmini ya mara kwa mara ya mwenendo wa uzalishaji, usambazaji na bei za bidhaa muhimu nchini zikiwamo vyakula, sukari, mafuta ya kula na vifaa vya ujenzi hususani saruji, mabati na nondo.

Pia amesema tathmini ilifanyika katika mikoa tisa inayotumia zaidi bidhaa hizo ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza, Pwani, Shinyanga na Ruvuma.

Akizungumzia kuhusu saruji alisema nchi ina viwanda tisa vinavyozalisha bidhaa hiyo vyenye uwezo wa kuzalisha tani 9,080,000 kwa mwaka. Alisema matokeo ya tathmini yanaonyesha kuwa katika mikoa hiyo bei za saruji zimepanda kwa wastani wa Sh. 1,000.

Alitolea mfano mkoa wa Mwanza ambao bei imeongezeka kutoka Sh. 19,000 kwa mfuko wa kilo 50 kwa Septemba hadi kufikia Sh. 20,000 mwezi Novemba.

Pia kwa mkoa wa Dar es Salaam, alisema  bei imepanda kutoka Sh. 14,000 kwa mwezi Septemba hadi Sh. 15,000 Novemba mwaka huu huku Ruvuma bei ikishuka kwa asilimia 15 kutoka Sh. 17,000 hadi 14,500 kwa kipindi hicho.

“Kupanda kwa bei za saruji katika kipindi cha tathmini kulisababishwa na mfumo wa usambazaji wa bidhaa hiyo na hakutokani na kupanda kwa gharama za uzalishaji viwandani. Kwa sababu hiyo ongezeko la bei linachukuliwa kuwa halikuwa halali,” amesema Prof. Mkumbo.