Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 28Article 560077

Habari za Afya of Tuesday, 28 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mambo matano yatakayowapima ubora wa Madaktari nchini

Mambo matano yatakayowapima ubora wa Madaktari nchini Mambo matano yatakayowapima ubora wa Madaktari nchini

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi, amesema waganga wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa watapimwa kwenye utendaji kazi wao kwenye mambo matano, ikiwamo utekelezaji wa maagizo ya viongozi wa juu.

Alisema hayo jana jijini hapa katika kikao na waganga wafawidhi hao.

Alisema utendaji kazi wa waganga wafawidhi wa hospitali za mikoa utapimwa kwa kuangalia uwajibikaji, uongozi, uzalendo na ubunifu kwa kufanya vikao vingi na kushirikisha wafanyakazi katika mambo mbalimbali.

Alisema pia watapimwa katika ukusanyaji wa mapato, uwajibikaji, uboreshaji wa huduma na kushughulikia malalamiko ya wagonjwa.

"Tutakuwa tunawapima jinsi gani unavyoboresha huduma zako mtu akifika anaona ubora. Pia mapato, unapoboresha mapato unafikia malengo na jinsi unavyoshughulikia malalamiko ya wananchi. Malalamiko mengi yamepungua sana, mwaka jana kila siku ilikuwa ni malalamiko sasa hivi yamebaki wilayani," alisema.

Profesa Makubi alisema watawapima waganga hao jinsi wanavyotekeleza maagizo kutoka kwa viongozi wa juu kama vile Rais na Waziri Mkuu.

"Utakuta mwingine anapuuzia tu maagizo ya Rais au Waziri Mkuu au miongozo inayoletwa, baada ya mwezi unaambiwa ulete ripoti huleti."

"Masuala ya ubunifu nayo tunayaangalia, kutogombana na wafanyakazi wenzako, tunategemea ninyi ndio mna jukumu kubwa la kubeba mikoa kuhakikisha huduma zinakuwa bora pamoja na kuondoa malalamiko na nyinyi ndio wasimamizi wa hizo hospitali," alisema.

Aidha, Profesa Makubi alisema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuendelea kuboresha huduma za tiba na kinga ikiwamo kupanua huduma za kibingwa katika hospitali za wilaya.

Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia magonjwa yasiyoyakuambukiza wa wizara hiyo, Dk James Kiologwe, aliwataka waganga hao kupeleka mipango mikakati yao wizarani kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya ugonjwa wa Covid-19 ambao umekuwa ukisababisha kero kadhaa pamoja na suala la maadili kwa wafanyakazi kushuka.