Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 28Article 560140

Habari Kuu of Tuesday, 28 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Mameneja TANESCO presha juu panga pangua ya Wizara

Panga pangua ya Tanesco yawaweka juu watendaji na Mameneja Panga pangua ya Tanesco yawaweka juu watendaji na Mameneja

Mabadiliko makubwa ya kiutawala yaliyofanywa ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) sio tu yamewashtua vigogo, bali hata wafanyakazi wa kada mbalimbali ndani ya shirika hilo wamepigwa butwaa.

Juzi, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko kwa kumng’oa Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Dk Alex Kyaruzi na kumteua aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Multichoice Africa inayomiliki ving’amuzi vya DSTv, Maharage Chande na Omari Issa kuwa mwenyekiti mpya wa bodi ya shirika hilo.

Mbali na vigogo hao, pia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga aliwahamisha vituo vya kazi vigogo watano wa shirika hilo ambao watasubiri kupangiwa majukumu mengine.

Waliohamishwa ni Naibu Mkurugenzi wa Uwekezaji, Khalid James, Naibu Mkurugenzi Usambazaji na Masoko, Taymond Seya, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji, Isaac Chanje, Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Nyelu Mwamaja na Amos Ndege ambaye ni Mwanasheria wa Tanesco. Vigogo hao wamepelekwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kusubiri majukumu mengine, huku Serikali ikijipanga kuziba nafasi zao kwa kuteua wengine watakaomsaidia Chande.

Hata hivyo, kung’olewa kwa vigogo ndani ya shirika kumepokelewa kwa namna tofauti na wafanyakazi wa shirika hilo. Baadhi ya watumishi waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina gazetini walisema mabadiliko hayo ni makubwa na hayajawahi kutokea ndani ya shirika hilo. Walisema kwa muda mrefu yamekuwa yakifanyika mabadiliko ya kawaida yanayohusisha vigogo wachache, lakini kilichotokea juzi ni mtikisiko ndani ya Tanesco.

Hata hivyo, watumishi hao wamekwenda mbali zaidi kwa kueleza bado hawaelewi mwisho wa mabadiliko hayo na wengine wameanza kupata hofu na nafasi zao za uongozi.

“Kiukweli hali sio shwari kabisa, hapa Dar kila mtu ni kama amechanganyikiwa kwa mabadiliko haya. Tumezoea kuona mabadiliko ya mara kwa mara ya kubadilishwa mkurugenzi, lakini hiki kilichotokea hatukukitarajia, nadhani tangu shirika kuanzishwa. Hapa ni uongozi mzima wa juu umeondolewa, hivyo Tanesco inakwenda kuanza upya ikiwa na menejimenti na bodi mpya. “Kinachotia hofu ni kuwa hakuna anayefahamu hawa jamaa wataingia hapa na mikakati gani na watatumia mfumo gani kuongoza shirika, lakini kwangu niko tayari kwa kuwa nipo hapa kwa ajili ya kazi na vyeti vyangu ndio vimenileta hapa...sijaletwa na mtu,” alisema mmoja wa wafanyakazi anayehudumu kwenye kitengo cha huduma za dharura.

Mfanyakazi mwingine kutoka mkoa wa Kanda ya Ziwa, alisema uamuzi wa Serikali kuwaondoa idadi kubwa ya viongozi wanaounda menejimenti, kunalenga kulisuka upya na kutoa huduma kwa ufanisi zaidi kwa wananchi.

Hata hivyo, alisema hofu zaidi imeanza kutanda kwa wakuu wa vitengo na mameneja wa mikoa na wilaya ambao ndio watekelezaji wakubwa wa maelekezo kutoka juu.

Alisema kwa hali ilivyo sasa, ni dhahiri hakuna meneja mwenye uhakika na nafasi yake ndani ya shirika. Hata hivyo, hali hiyo ni tofauti kwa wafanyakazi wa ngazi ya chini ambao baadhi wameonyesha kuguswa na mabadiliko hayo wakisema yatasaidia kulirejesha shirika kwenye mstari na kufanya kazi kisasa zaidi.

“Kuna wakati mabadiliko hayaepukiki sehemu za kazi, naliona lengo la Serikali na aina ya watu walioteuliwa ni kulifanya Tanesco kufanya kazi kisasa zaidi. Ukiangalia wajumbe wapya wa bodi si watu wa njaa na ni mwagwiji katika taaluma. Sina shaka kabisa, ila balaa liko huko kwa mameneja ambako kuna baadhi hawajui hatima zao. Nina uhakika kwa hali ilivyo, pangua pangua itafika huko na kuna wengine hasa wale wa kufanya kazi kwa mazoezi, mambo yatakuwa magumu sana kwao,” alisema mfanyakazi huyo ambaye pia aliomba kuhifadhiwa jina.

Wakati Chande akitarajiwa kuanza kazi leo na kunadi mikakati yake kwa watendaji waliobaki na wafanyakazi kulingana na ratiba zake, jana alikuwa na kikao na viongozi wengine wakikutana na Waziri wa Nishati, Januari Makamba.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Meneja Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki, Mhandisi Soti Konombo alisema amepokea maagizo ya waziri na kuahidi kumpa ushirikiano, ili malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi yatimie. Meneja Mwandimizi wa Kanda ya Kati, Frank Chambua alimpongeza Makamba kwa hotuba yake akisema imemrahisishia utekelezaji wa majukumu yake na kwamba ndani ya muda mfupi matokeo yataonekana.