Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572707

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: Habarileo

Maoni ya wanazuoni kuhusu utayari wa Tanzania kuingia uchumi wa viwanda

Maoni ya wanazuoni kuhusu utayari wa Tanzania kuingia uchumi wa viwanda Maoni ya wanazuoni kuhusu utayari wa Tanzania kuingia uchumi wa viwanda

WANAZUONI wamebainisha kuwa Tanzania iko tayari kushiriki mapinduzi ya viwanda baada ya kuwekwa mazingira wezeshi. Akiwasilisha mada kwenye mkutano wa kitaaluma ulioandaliwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MOCU), Profesa Alfred Side alisema kwa sasa serikali imeweka miundombinu wezeshi kwa Tanzania kushiriki vyema kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda.

“Tayari miundombinu ya kisera, kisheria, utashi wa kisiasa na hata teknolojia na mifumo imeshaandaliwa, jambo ambalo linaashiria kuwa Tanzania iko tayari kuingia kwenye uchumi wa viwanda,” alisema.

Alisema kinachotakiwa sasa ni kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania kwenye uchumi wa viwanda kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda kwa kuboresha zaidi mitaala, kuongeza ufikiwaji wa huduma za kidijiti na kuongeza matumizi ya data na vifaa vya Tehama hususani maeneo ya vijijini.

Mkutano huo wa siku mbili umehudhuriwa na watafiti kutoka ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara na wanazuoni zaidi ya 300. Awali, Mkuu wa CBE, Profesa Emmanuely Mjema alisema chuo kimekuwa kikishiriki azma ya serikali ya uchumi wa viwanda kwa kufanya makongamano, tafiti, mafunzo na ushauri wa kitaalamu katika sekta ya viwanda.

Mwenyekiti wa kongamano hilo, Dk Dickson Pastory alisema katika mkutano huo tafiti zaidi ya 80 zimewasilishwa na kujadiliwa. Zimejikita katika maeneo ya ubunifu na ujasiriamali, uchumi na maendeleo endelevu, fedha na biashara, uchumi wa kidijitali, biashara za kimataifa, Tehama na biashara, elimu ya biashara na fursa za uwekezaji.