Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 30Article 560563

Uhalifu & Adhabu of Thursday, 30 September 2021

Chanzo: IPPmedia

Mashahidi wa Jamuhuri kuongezeka kesi ya Sabaya na wenzake

Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai

Kesi ya uhujumu uchumi namba 27, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita, inatarajiwa kuendelea kunguruma leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, ambapo mashahidi wa Jamhuri watatoa ushahidi.

Washtakiwa wengine ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Septemba 23, mwaka huu akitoa ushahidi, aliyekuwa Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Renatus Msangira (45), alidai kwamba Ole Sabaya, hakupewa kibali chochote cha maandishi kwenda kutekeleza majukumu nje ya kituo chake cha kazi.

Msangira, ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, alitoa madai hayo, wakati akitoa ushahidi, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Filex Kwetukia.

Alidai kiutaratibu Mkuu wa Wilaya akitaka kwenda kufanya kazi nje ya kituo chake cha kazi inatakiwa apate kibali cha maandishi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, lakini hilo halikufanyika.

Naye shahidi wa pili wa Jamhuri, ambaye ni Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Arusha, Kayobio Majogoro(41), alidai ofisi yake, haikuwa na taarifa za Sabaya, kuongoza kikosi maalum kwenda kufanya operesheni ya kukusanya kodi jijini Arusha.

Septemba 24, mwaka huu, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmed Mtenga, alidai kwa mujibu wa sheria, Kamishna Mkuu wa TRA, ndiye mwenye mamlaka ya kuunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kukusanya na kuchunguza masuala ya kikodi.

Majogoro alidai suala na kukusanya kodi lipo chini ya mamlaka hiyo na wakuu wa wilaya hawahusiki kukusanya kodi, bali wanabaki kuwa kama wadau wa taasisi hiyo ya serikali.

Alidai vyombo vingine vya dola wakiwamo askari wanashirikiana nao kwa kuwaomba msaada kama wanakwenda kufanya operesheni maalum ya kukusanya kodi au kufanya uchunguzi.

Katika kesi hiyo, shtaka la kwanza ni la kuongoza genge la uhalifu kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi Kifungu cha 57(1) na 60(2) na linawakabili washtakiwa wote.

Ilidaiwa kwa pamoja washtakiwa hao, Januari 22, mwaka huu katika maeneo tofauti ya Jiji la Arusha, akiwa mtumishi wa serikali kwa nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, walifanya vitendo vya uhalifu kwa kujipatia fedha kiasi cha Sh. milioni 90 kwa manufaa yao.

Shtaka la pili ni la kujihusisha na vitendo vya rushwa na linamkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake.

Ilidaiwa Januari 22, mwaka huu, eneo la kwa Murombo jijini Arusha, Sabaya alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kumtaka Francis Mrosso, kumpatia Sh. milioni 90 kwa kumshinikiza ili asitoe taarifa za jinai za mtu huyo za madai ya ukwepaji kodi.

Shtaka la tatu ni la kujihusisha na vitendo vya ruswa linamkabili Sabaya, ambapo ilidai Januari 22, mwaka huu, akiwa katika eneo la kwa Morombo jijini Arusha, alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kujipatia Sh. milioni 90, kutoka kwa Francis Mrosso, ili asitoe taarifa za jinai za mtu huyo za madai ya ukwepaji kodi.

Shtaka la nne ni la matumizi mabaya ya madaraka, linamkabili Sabaya peke yake, ambapo ilidaiwa kuwa, Januari 22 mwaka huu, akiwa katika eneo la kwa Murombo, alitumia vibaya nafasi yake ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, kwa kumtisha Francis Mrosso, kumfungulia mashtaka ya kukwepa kodi

Shtaka la tano ni la utakatishaji wa fedha na linawakabili washtakiwa wote saba, Inadaiwa Februari 22, mwaka huu, Ole Sabaya kwa kushirikiana na wenzake, wakiwa katika eneo la kwa Murombo Jijini Arusha, walijipatia Sh.milioni 90, wakitambua kufanya hivyo ilikuwa ni zao la vitendo vya rushwa.