Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 11Article 542179

Habari Kuu of Friday, 11 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Masomo ya sayansi kufundishwa kwa Tehama

Masomo ya sayansi  kufundishwa kwa Tehama Masomo ya sayansi kufundishwa kwa Tehama

WAZIRI wa Tamisemi, Ummy Mwalimu amesema wizara yake itatumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuwawezesha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kupitia mtandao kutokana na uhaba wa walimu wa masomo hayo katika shule za sekondari nchini.

Alisema hayo bungeni Dodoma jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mchafu (CCM).

Mchafu alitaka kujua ni lini serikali itapeleka walimu wa shule za sekondari katika shule za halmashauri zote za mkoa wa Pwani.

Ummy alisema sambamba na kuomba kibali kuajiri walimu kutoka Ofisi ya Rais Utumishi, wizara yake itatumia Tehama kufundisha masomo ya sayansi ili kuwawezesha wanafunzi kupata masomo hayo kupitia mtandao.

“Tutaweka walimu kurekodi masomo wanayofundisha na wanafunzi wataweza kusoma masomo mbalimbali yakiwamo ya sayansi kupitia mtandao,” alisema.

Ummy alisema kuna changamoto ya uhaba wa walimu wa sayansi kwani uchambuzi waliofanya miezi mitatu umebaini kwamba wanafunzi takribani 1,000 hawajawahi kukutana na mwalimu wa fizikia uso kwa uso.

“Katika uchunguzi huo tumebaini kwamba shule takribani 400 hazijawahi kumwona mwalimu wa hesabu darasani, hivyo wizara imeliona tatizo hilo,” alisema.

Ummy alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu walimu kuajiriwa katika mwaka wa fedha 2020/21 na kwamba wizara hiyo inaendelea kukamilisha uchambuzi wa maombi na kipaumbele ni kutatua changamoto ya walimu wa hesabu.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Davidi Silinde wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini, Zacharia Issaay (CCM), alisema serikali inaendelea kuratibu utaratibu wa kuajiri walimu 6,949 katika ajira zilizotangazwa Mei, mwaka huu ambao watapangwa kwenye shule mbalimbali nchini zikiwamo za halmashauri ya Mji wa Mbulu.

Alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi 20219/20, serikali imeajiri na kuwapanga walimu 17 wa masomo ya sayansi na hisabati na mafundi sanifu wa maabara wawili katika shule za halmashauri ya Mji wa Mbulu.

“Walimu na mafundi sanifu wa maabara ni kati ya walimu

10, 418 wa sekondari na mafundi sanifu maabara 397 walioajiriwa katika kipindi hicho nchini,” alisema.

Join our Newsletter