Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 04Article 561247

Habari za Mikoani of Monday, 4 October 2021

Chanzo: ippmedia.com

Matukio ukatili kijinsia kwa watoto Babati yaongezeka

Matukio ukatili kijinsia kwa watoto Babati yaongezeka Matukio ukatili kijinsia kwa watoto Babati yaongezeka

SERIKALI imesema matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, yanaongezeka kila uchao na kutishia ustawi wao.

Inaelezwa kuwa katika halmashauri hiyo, watoto 15 hadi 20 wanaripotiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili na wazazi wao au ndugu zao wa karibu kila mwaka.

Kwa mujibu wa Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mathias Focus, matukio hayo kwa sasa yanaongeza wasiwasi, licha ya kuwa serikali na mashirika mbalimbali ya haki za binadamu yanapigana kufa na kupona kupinga matukio hayo, kueleza madhara na kutoa elimu ya namna ya kuyakabili.

Aliyataja makundi yanayoongoza kwa kufanyiwa ukatili ni watoto kuanzia miaka sifuri hadi miaka 15, yakifuatiwa na wanawake na wazee.

“Ukatili unaofanywa kwa watoto mara nyingi ni ule wa kutelekezwa na wazazi wao, kupigwa, kumwagiwa maji ya moto, kutukanwa, kubakwa na kulawitiwa.

“Kwa mfano matukio yanayotokea Babati ni mengi ila yanayoripotiwa ni machache na tunayomaliza kwa kujadiliana ni machache. Mengi ni ya jinai tunayapeleka mahakamani.”

Alitumia fursa hiyo kuionya jamii, kuacha kujichukulia sheria mkononi ya kuwajeruhi na wakati mwingine kuwasababishia mauti kutokana na hasira.

"Mtoto anapaswa kuelekezwa na siyo kwa kutumia nguvu kwa kumpiga au kumfinya au kutumia maneno makali ambayo yanamwathiri kisaikolojia," alisisitiza.

Mkazi wa Mtaa wa Maisaka A, Yusta Shemdoe, alisema chanzo cha ukatili mara nyingi ni watu kukosa roho ya Mungu ambayo ndio inaleta upendo.

Yusta alifafanua kuwa watu wanaowafanyia ukatili watoto wengi wakifatiliwa wanaweza wakakutwa nao walikuwa wanafanyiwa hivyo na sasa wanalipiza.

Mkazi wa Mtaa wa Negamsi, Paul Mshana, akizungumza na Nipashe alisema serikali imekuwa ikiwahukumu watu wanaolawiti na kubaka watoto ila wanaowafanyia ukatili wa kuwatukana, kuwafinya na kuwakebehi hawachukuliwi hatua.