Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 22Article 543721

Habari Kuu of Tuesday, 22 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mawaziri leo kujibu hoja zilizotikisa bajeti

Mawaziri leo kujibu hoja zilizotikisa bajeti Mawaziri leo kujibu hoja zilizotikisa bajeti

LEO wabunge wanatarajiwa kupitisha bajeti ya serikali ya Sh trilioni 36.33 kwa mwaka 2021/22.

Kabla ya wabunge kupiga kura ya wazi bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba atajibu hoja za wawakilishi hao wa wananchi.

Wakati wabunge wakijadili bajeti hiyo iliyowasilishwa Juni 10, mwaka huu, mambo kadhaa yalizungumzwa zaidi na wabunge zikiwemo pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kwa kiwango kikubwa imejibu kero za wananchi.

Wabunge pia walimpongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kutenga fedha kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa kufua umeme katika Bwawa la Mwalimu Nyerere (JKHPP) na miradi mingine iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Wawakilishi hao wa wananchi pia walipongeza uamuzi wa serikali wa kuwalipa madiwani posho za Sh 100,000 kutoka mfuko mkuu wa serikali badala ya kulipwa na halmashauri.

Wabunge pia waliipongeza serikali kutafuta chanzo kipya cha kukata Sh 100 kila lita ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kusaidia Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) kupata fedha za kujenga na kuboresha barabara vijijini.

Pia waliipongeza serikali kwa kutoa fedha kwa kila jimbo kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika majimbo ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu, mazao na mizigo.

Bunge na wabunge kwa umoja wao walipongeza uamuzi wa serikali kipunguza faini za bodaboda na bajaji kutoka Sh 30,000 hadi Sh 10,000 ili kuwainua vijana hao kufikia kumiliki bodaboda zao.

Wabunge waliipongeza serikali katika kutafuta njia bora ya kukusanya kodi ya majengo kupitia mita za umeme la LUKU (Lipia Umeme kadiri Unavyotumia) kwa maana kwamba kila mtumiaji wa ememe atalipia kodi ya jengo analomiliki.

Pia walijadili kuhusu uamuzi wa serikali wa kutoza kwenye huduma za matumizi ya simu kwa ajili ya fedha hizo kukusanywa na kusaidia mkakati wa kuanzisha bima kwa wote na wakaomba fedha hizo ziwekewe zuio zisijetumika kwa kazi nyingine.

Wabunge pia walipongeza juhudi za serikali kuondoa Kodi ya Ongezeko la thamani (VAT) katika bidhaa mbalimbali yakiwemo majokofu kuhifadhia vyakula, mboga na huduma nyingine pamoja na kwenye nyasi bandia ili kuboresha viwanja katika majiji kwa kuanzia na baadaye katika miji mingine.

Mjadala ulikuwa mkali kuhusu bajeti ya kilimo wakitaka bajeti iongezwe kutoka bilioni 200 zilizotengwa kutokana na umuhimu wake kuajiri watanzania asilimia 65 na inategemewa kwa asilimia 100 katika kutoa chakula wakaomba uwekezaji zaidi unatakiwa katika kuanzisha mashamba makubwa na teknolojia ya kupima udongo itumike.