Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 27Article 540199

Habari za michezo of Thursday, 27 May 2021

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mawete, staa Simba asiyemchoka Samatta, Mugalu dimbani

Mawete, staa Simba asiyemchoka Samatta, Mugalu dimbani Mawete, staa Simba asiyemchoka Samatta, Mugalu dimbani

MIONGONI mwa silaha za kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi ni pamoja na Mawete Musolo (20), ambaye amekuwa akifanya vizuri sambamba na Opah Clement kwenye kikosi hicho.

Mawete ni mchezaji wa kigeni anayecheza kiungo mshambuliaji. Ukimtazama mwonekano wake huwezi kutarajia kama ni mchezaji kwa namna alivyo mrefu, mweusi, umbo zuri na muda wote anatabasamu.

Mawete hajui lugha ya Kiswahili wala Kiingereza, bali anafahamu lugha zinazotumika nchini kwao DR Congo ambazo ni Kilingala na Kifaransa, hivyo wakati wa mahojiano maalumu na Mwanaspoti msaada wa ukalimali ulifanywa na Jane Mhoza ‘Hadija’ ambaye ni kipa wa timu hiyo.

Hadija anazijua lugha hizo kwa sababu amewahi kucheza soka la kulipwa nchini DR Congo.

Mawete alizungumzia mambo mbalimbali katika soka analocheza hadi alipofika nchini kuitumikia timu hiyo.

SOKA LA TANZANIA

Kiungo huyo aliyetokea jijini Kinshasa, anasema maisha ya soka la Bongo ni mazuri, na amekuwa akiyafurahia tofauti na kwao ambako ligi imekuwa ikichezwa kwa mikoa.

“Huu mfumo wa kutembea sehemu mbalimbali nimeupenda sana, maana nyumbani ligi zinachezwa kwa mikoa. Navutiwa pia na ushindani uliopo Tanzania, ligi ni nzuri, ninajiona mwenye furaha kuwa hapa,” anasema Mawete.

“Naamini nilifanya uamuzi sahihi kujiunga na Simba Queens. Tangu nilipokuja Tanzania nimekuwa nikishirikiana vizuri na wenzangu pamoja na kukabiliwa na changamoto ya lugha, lakini nimekuwa nikijifunza taratibu na nina imani kwamba mambo yatakaa sawa.”

UHAMISHO ULIVYOKUWA

Aliyekuwa nyuma ya uhamisho wa kiungo huyo ni Hadija anayeeeleza kwamba baada ya kucheza kwa kipindi kirefu DR Congo na kurejea nyumbani kwao Rwanda, baadaye alitua Simba na kuwaeleza viongozi wa timu hiyo namna anavyomjua nyota huyo na kufanikisha dili hilo.

Huku Mawete akiwa kimya na kusikiliza bila ya kuelewa kile ambacho alikuwa akizungumza rafiki yake ambaye alitumia dakika mbili kuelezea sakata la uhamisho wa kiungo huyo.

“Namfahamu (Mawete) kuwa ni mmoja wa washambuliaji hatari kwa sababu nilicheza naye, baada ya mashindano ya Cecafa hapo ndipo Simba walimuona na kwa sababu nilikuwa nafahamiana naye walinitumia ili kusaidia upatikanaji wake. Nilifurahi kuungana naye tena baada ya usajili wake kukamilika,” anasema Hadija.

CHAPATI TAMU

Baada ya Hadija kueleza alivyohusika kwenye usajili wake, Mawete anaweka wazi chakula anachokipenda akiwa hapa Tanzania.

Baada ya kuulizwa kwa lugha anayoifahamu kisha akajibu, “chapati.” Kwanini? Hadija anafafanua, “Unajua kule DR Congo hakuna chapati pengine ndio maana amekuwa akizipenda sana, akila anafurahi sana.”

MUGALU NDO KILA KITU

Mawete anasema licha ya Simba kuwa na wachezaji wengi, lakini turufu yake anaitupa kwa Chris Mugalu ambaye kwa sasa ni moto wa kuotea mbali. “Napenda vile anavyocheza, kiukweli Simba kuna wachezaji wengi wazuri lakini Mugalu ndiye chaguo langu, namfuatilia sana,” anasema.“Sio kwa sababu ni Mkongomani mwenzangu, hapana. Napenda anavyocheza kwa nafasi, ana uwezo wa kukaa na mpira akisubiri wenzake wapande. Hilo nimekuwa nikijifunza kutoka kwake, tumekuwa tukiongea.”

SAMATTA BALAA

Mawete anamtaja mshambuliaji wake hatari wa Kitanzania kuwa ni nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta na amekuwa akimfuatilia kipindi kirefu tangu akiwa mdogo nchini kwao kabla hata kuaminiwa na kucheza soka la ushindani.

“Samatta ni mchezaji mzuri sana. Nilikuwa nikimsikia tangu akiwa TP Mazembe, alifanya makubwa na kuisaidia timu kutwaa ubingwa wa Afrika, ilikuwa furaha iliyoje kwetu kuona taji la Afrika linakuja nyumbani, nilisikitika alipoondoka na kwenda Ulaya, lakini ndio maisha ya mpira yalivyo.”

KISWAHILI VIPI?

Mawete anasema anatamani na anapenda kujua kuzungumza Kiswahili kwani anapata wakati mgumu pale anapohitaji kitu haraka wakati Hadija akiwa mbali naye.

“Najifunza kidogokidogo, nitakuja kujua kwa kuwa napenda sana kujua, ila kuna maneno nayajua kama pole, mambo, poa, nakuja, twende na nipe nitayajua mengi huko mbeleni,” anasema.

Mawete ambaye alijiunga na Simba Queens katika raundi ya pili ya Ligi Kuu ya Wanawake akitokea Eclat Sports amemaliza msimu akiwa amefunga mabao saba na lengo licha ya kujiunga raundi ya pili alitamani kufunga mabao mengi zaidi.

“Najituma ili niisaidie Simba Queens na timu yangu ya taifa ya Congo, natambua soka ni kazi niliyoichagua, hivyo nitaifanya kwa nguvu zangu zote.”