Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 12Article 585160

Uhalifu & Adhabu of Wednesday, 12 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Mazito zaidi anayedaiwa kumuua mama mzazi

Mazito zaidi anayedaiwa kumuua mama mzazi Mazito zaidi anayedaiwa kumuua mama mzazi

Mambo mazito yanazidi kufichuka katika tukio la mtoto wa kike anetuhumiwa kumuua mama yake mzazi aitwaye Patricia Ibreck na kufukia mwili wake kwenye shimo jirani na nyumba ya mama yake huyo nje kidogo ya mji wa Moshi.

Patricia (66) alikuwa muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Tukio hilo ambalo limekuwa gumzo katika mitaa mbalimbali ya mji wa Moshi na katika mitandao ya kijamii, linadaiwa kutokea katika kijiji cha Rau Mrukuti Februari mwaka jana, lakini mtoto akaficha mauaji hayo kwa mwaka mzima.

Kabla ya mauaji hayo, mtoto wa marehemu aitwaye Wendrin Ibreck ambaye ni miongoni mwa wanaoshikiliwa na polisi, anadaiwa aliwaalika waganga wawili wa jadi ili kumtibu marehemu na katika harakati hizo, waganga hao walichota Sh60 milioni.

Kamanda wa Polisi mkoa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema jana kuwa marehemu alishtuka kuwa anatapeliwa kwa vile zimeshatumika Sh60 milioni na haoni matumaini ya kupona, ndipo waganga na mtoto walipodaiwa kupanga mauaji.

‘‘Kila ndugu walipokuwa wanaulizia mama yake yuko wapi, aliwajibu kuwa alikuwa amesafiri kwenda nchini India kwa matibabu, lakini wakati huo alianza kuuza mashamba kwa kasi jambo ambalo liliwafanya ndugu kutilia mashaka,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, baada ya upelelezi kufanyika, Jeshi la Polisi lilimtia mbaroni mtoto wa marehemu na waganga wawili, mmoja mkazi wa Dar es Salaam na mmoja wa mkoani Tanga, wakihusishwa na mauaji hayo.

Kamanda Maigwa aliwaeleza wanahabari jana kuwa mmoja wa waganga hao alikuwa na uhusiano ya kimapenzi na binti wa marehemu ambaye naye anadaiwa kuwa mshiriki wa kupanga na kushiriki katika tukio hilo la mauaji.

“Mama huyo alianza kushtuka baada ya kuona fedha zaidi ya Sh 60 Milioni za kustaafu zimeshatumika lakini haoni matumaini ya kupona, wakati huo waganga hao kwa kushirikiana na binti yake wakitaka aendelee kutoa fedha,”alisema.

“Kutokana na hali hiyo, mama huyo hakuridhika na kuona kama kuna vitendo vya kitapeli vinavyofanywa na hao waganga kwa kushirikiana na binti yake na katika mabishano, ndipo watuhumiwa walipoamua kumuua”

“Walimuua nyumbani kwa mama huyo na baadaye kumhifadhi katika moja ya vyumba vya nyumba hiyo kusubiri giza liingie, lilipoingia waliuchukua ule mwili na kwenda kuufukia kwa lengo la kuuficha, ‘‘ alieleza.

Alieleza kuwa matendo ya binti yake huyo yalianza kuwajengea shaka ndugu na majirani kwa sababu alianza kuuza mali za nyumbani kwao na hususan ardhi na alipoulizwa alidai fedha zinazopatikana anazipeleka India kwa ajili ya matibabu ya mama yake.

“Kitendo hicho kiliwajengea wananchi mashaka na Disemba21, 2021 taarifa zilifika kituo cha polisi baada ya miezi 10 kupita tangu mama huyo kudaiwa kupotea na tulianza upelelezi ikiwamo kukusanya ushahidi na vielelezo,”alieleza.

Kamanda Maigwa alisema baada ya kuhojiwa na makachero wa Polisi, watuhumiwa wanadaiwa kukiri kuhusika na mauaji hayo na walikuwa tayari kwenda kuonyesha mahali walipofukia mwili.

“Baada ya kufika eneo la tukio mabaki ya marehemu yalifukuliwa Januari 9, 2022, katika eneo hilo ambalo ni sehemu ya eneo la familia na ndani pia lilikutwa panga lililokuwa na nywele zinazoaminika ni za marehemu,”alieleza Kamanda.

Kamanda Maigwa alisema mabaki hayo yamehifadhiwa hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa kisayansi ili kujiridhisha kama ni mabaki ya binadamu.