Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 24Article 559546

Habari za Afya of Friday, 24 September 2021

Chanzo: Mwananchi

Mbeya yaanza kutoa chanjo nyumba kwa nyumba

Chanjo Chanjo

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ametangaza kuanza utoaji wa chanjo ya Uviko 19 nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda na katika nyumba za ibada kuazia kesho Jumamosi Septemba 25, 2021.

Homera ametoa msimamo huo leo Ijumaa Septemba 24, 2021 kwenye kikao cha wadau cha uhamasishaji wa chanjo kwa wananchi mkoani Mbeya.

Amesema wamefikia uamuzi huo kwa sababu Mkoa ulipokea chanjo 50,000 lakini mpaka sasa waliopata chanjo ni 10,000 jambo ambalo halikubaliki huku Serikali ikiwa imetumia gharama kubwa kwa lengo la kuokoa uhai wa Watanzania

"Zoezi la utoaji chanjo ya Uviko 19 ni nyumba kwa nyumba ,kitanda kwa kitanda kwa kuwashirikisha watendaji wa ngazi za kata na vijijini kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa na jamii kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa uviko 19 ingawa sio lazima lakini itabidi iwe hivyo,"amesema.

Mwakilishi wa Wizara ya Afya, Dk Baraka Nzobo amesema jamii inapaswa kutambua chanjo hiyo haina madhara kwa binadamu na kwamba inasaidia kupunguza vifo na maambukizi ya Uviko 19.

"Ni hofu tu imejengeka miongoni mwa jamii na tafsiri tofauti juu ya kinga hiyo hivyo niungane na mkuu wa mkoa kwa kuanza kwa zoezi la nyumba kwa nyumba ,kitanda kwa kitanda ili kufikia malengo ya serikali ya chanjo zikizotolewa katika kila mkoa."amesema.

Mkazi wa Forest, Saada Abdalla amesema msimamo huo wa Homera ni sahihi kwani jamii imekuwa ikiona chanjo hiyo ni kama sumu jambo ambalo linachangia kuwepo kwa vifo vitokanavyo na Uviko 19 na kuwepo kwa changamoto ya vifaa hususan oksijeni kwenye hosptali zetu nchini.