Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 15Article 542794

Siasa of Tuesday, 15 June 2021

Chanzo: ippmedia.com

Mbowe awataja wachawi wa CHADEMA

Mbowe awataja wachawi wa CHADEMA Mbowe awataja wachawi wa CHADEMA

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, aliyasema hayo jijini Mbeya wakati wa mkutano wa ndani wa wanachama wa chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Nyasa), uliolenga kutoa elimu ya kuhusu mageuzi ya kidijitali.

Alisema mara nyingi wamekuwa wakishindwa kwenye chaguzi wanasingizia kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala kiliiba kura na baadhi wakidai kuonewa na serikali, lakini ukweli ni kwamba katika baadhi ya maeneo sio kweli.

Alisema baadhi ya viongozi wa chama hicho wamekuwa wakifanya kazi kwa maslahi yao binafsi, lakini kazi za chama hawashiriki, hali ambayo inakifanya chama hicho kukosa nguvu katika maeneo husika.

“Nataka tuachane na kila makosa yetu tunayasukumia CCM, utasikia mtu anasema CCM waliiba kura, CCM waliiba uchaguzi. Ni kweli wanaiba, lakini kuna maeneo kadha wa kadha ambayo tunashindwa kwa sababu ya uzembe na uvivu wetu wenyewe,” alisema Mbowe.

Alisema ili chama hicho kifanikiwe kukiondoa CCM madarakani, ni lazima kijisahihihishe kwenye maeneo yote ambayo kilikuwa kinafanya makosa ikiwamo kufanya kazi ya kutafuta wanachama usiku na mchana.

Alisema kwa sasa baada ya kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kusajili wanachama, chama hicho kitafika kwenye uchaguzi mkuu ujao kikiwa kinajitegemea kiuchumi bila kutegemea ruzuku ya serikali, na kwamba kazi ya kuing’oa serikali ya CCM madarakani itakuwa ya kudumu.

Aliwataka wanachama wa chama hicho kuanza maandalizi mapema ya kumpata mgombea wa nafasi ya urais na nafasi zingine mapema kabla ya mwaka wa uchaguzi, badala ya kuanza harakati za kuwapata wagombea miezi michache kabla ya uchaguzi.

AMFAGILIA SAMIA

 

Katika hatua nyingine, Mbowe alisema chama hicho kitaendelea kumpa ushirikiano Rais Samia Suluhu Hassan, kwa maelezo kuwa serikali yake inafanya kazi vizuri.

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alisema chama hicho bado kipo imara katika Jiji hilo, na kwamba wananchi wanakikubali kuliko hata ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Alisema Jimbo la Mbeya Mjini litaendelea kuwa ngome ya chama hicho pamoja na kwamba kwa sasa lipo chini ya CCM, na akawataka wanachama kuendelea kujiandikisha kwenye mfumo wa kidigitali.

Sugu alisema kwa sasa CHADEMA haiko tayari kupokea ruzuku ya serikali, kwa maelezo kuwa ni haramu badala yake wataendelea kutumia nguvu za wanachama kukiendesha chama.

“Kuna wale wenzetu ambao waliamua kuungana na serikali, wao wamepewa vyeo, lakini sisi tumebaki na heshima na hiyo heshima ndiyo silaha yetu kubwa,” alisema Sugu.

Alimwomba Rais Samia kukutana na vyama vyote vya siasa kwa madai kuwa vyama hivyo ni miongoni mwa wadau muhimu wa maendeleo nchini.