Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540658

xxxxxxxxxxx of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mfuko UDSM kusomesha wageni shahada Kiswahili

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimeanzisha mfuko wa kusomesha wanafunzi kutoka nje ya nchi wanaotaka kusoma Shahada ya Uzamili katika Kiswahili.

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye alisema jana kuwa hadi sasa chuo hicho kimeanza katika nchi tatu za Ghana, Rwanda na Uganda.

Profesa Anangisye alisema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLEO kuhusu mchango wa chuo hicho kuhamasisha utumiaji wa Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Alisema uanzishwaji wa mfuko huo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayotaka kuhamasisha utumiaji wa Kiswahili kwa wageni kutoka nje ya nchi.

Profesa Anangisye alisema pia UDSM ipo kwenye mazungumzo ya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili katika vyuo vikuu vya Juba Sudan ya Kusini pamoja na Adis Ababa Ethiopia.

"Kama chuo tuna rasilimali watu, tuna rasilimali pesa, tuna vitabu na wataalam hivyo lengo letu ni kueneza lugha ya Kiswahili dunian. UDSM kipo mstari wa mbele kuhakikisha Kiswahili kinasambaa si kwa maneno, bali kwa kuonesha vitendo," alisema.

Anangisye alisema kwa miaka mingi chuo kikuu hicho kimekuwa kikifundisha kozi fupi fupi za Kiswahili kwa raia wa kigeni kutoka Marekani, Ujerumani, China, Japan na nchi nyingine, lakini sasa wameanzisha Shahada ya Uzamili.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) chuoni hapo, Dk Ernesta Mosha, alisema katika ngazi ya vyuo, chuo kikuu hicho kina mikataba na vyuo kikiwepo cha Napol Italia.

Alisema mkataba huo unahusu kubadilishana maarifa kuhusu Kiswahili na wakati mwingine, wanafunzi wa Napol wanakwenda UDSM ama wanapowataka walimu kutoka chuo hicho huenda Italia.

"Pia tunaandaa makongamano kwa pamoja. Lugha hii inafundishwa nchi nyingi katika kiwango cha chuo kikuu," alisema na kuongeza kuwa UDSM wamekuwa kinara katika kuandaa wataalam katika idara zote. “UDSM ni kitovu cha kukuza na kueneza Kiswahili hata nje ya nchi," alisema.

Mkurugenzi Umataifishaji, Jumuiya ya Wahitimu na Uendelezi UDSM, Dk Lulu Kaaya, alisema wamekuwa wakiingia mikataba na vyuo vya nje kuleta wanafunzi kujifunza Kiswahili ili wakirudi kwao, wakafanye kazi kwenye vyuo vyao alitoa mfano chuo cha Ghana ambao wapo kwenye mkataba huo kwa miaka 20 sasa.

"Lakini pia UDSM kimekuwa kikitafuta vyuo na kuingia nao mkataba wa kupeleka walimu wao kwa kufundisha katika level mbalimbali. Tupo kwenye mchakato huo na Chuo Kikuu cha Juba Sudan ya Kusini pamoja na Addis Ababa nchini Ethiopia ambapo bado hatujaanza kufundisha," alisema.

Alisema wanategemeoa katika mwaka wa masomo ujao, watakuwa wameanza angalau kwa nchi mojawapo kati ya hizo mbili.

Alisema hivi sasa UDSM inajitahidi kupunguza gharama za wanafunzi wa kigeni kusoma Kiswahili kwani wanasoma kwa ada sawa na Watanzania.

Juzi Waziri wa Habari, Utamadui, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alisema Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), limeandaa programu inayoitwa Swahili Prime itakayoanza Juni mwaka huu kufundishia Kiswahili kwa njia ya mtandao.

Bashungwa alisema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo ya mwaka wa fedha 2021/2022.

Alisema matumizi ya Kiswahili yanaongezeka kwa kasi duniani na kwamba, kukubalika kwa lugha hii kunachagizwa na mambo mbalimbali ikiweom msukumo wa kustawisha Kiswahili ndani na nje ya nchi uliofanywa na unaoendelea kufanywa na viongozi wa kitaifa.

Join our Newsletter