Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540403

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mfumo wa kielektroniki wa uhamisho watumishi kuanza kutumika Julai Mosi  

KUANZIA Julai Mosi, 2021 mfumo mpya wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara utatumika kuchakata na kuoanisha maombi ya vibali vya uhamisho wa Watumishi wa Umma ili kupunguza malalamiko ya watumishi kuhusu changamoto iliyopo ya upatikanaji wa vibali vya uhamisho kuchukua muda mrefu,” Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk Laurean Ndumbaro amesema kuanzia

Dk Ndumbaro amesema hayo leo mjini Sumbawanga wakati akizungumza na watumishi mkoani Rukwa wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma mkoani humo.

Dk Ndumbaro amesisitiza kuwa, mfumo huo utakapoanza kufanya kazi, utaboresha ufanisi wa waajiri katika kuratibu zoezi zima la uhamisho wa Watumishi wa Umma nchini.

“Baada ya watumishi kuomba uhamisho, maombi yote yataingizwa kwenye mfumo ambapo yatachakatwa, kuoanishwa na kuwasilisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kutoa kibali,” Dk Ndumbaro amefafanua.

Dk Ndumbaro amefafanua kuwa, ili kuhakikisha uhamisho hauibui tatizo la uhaba wa watumishi kwenye maeneo ya uhitaji mkubwa wa rasilimaliwatu, Wakuu wa Taasisi za Umma, Wakurugenzi Watendaji, Matatibu Tawala Mkoa, Katibu Mkuu TAMISEMI pamoja yeye mwenyewe wamepewa uwezo wa kuona na kuratibu maombi yote ya uhamisho ndani ya maeneo yao ya utawala, hivyo suala la uhamisho litakuwa rahisi kufanyiwa kazi na mamlaka, kwa mantiki hiyo watumishi wataruhusiwa kuhama pasipokuwa na vikwazo visivyo na msingi wowote.

Kwa upande wake Mtumishi Kilingo ambaye ni Mwalimu, ameipongeza Serikali kwa kuunda mfumo utakaoratibu uhamisho na malipo ya madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi (automatic) na kuongeza kuwa mfumo huo utapunguza kero zilizokuwa zikiwakabili Watumishi wa Umma nchini kwa kipindi kirefu.

Dk Ndumbaro amehitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Rukwa na kuelekea mkoani Katavi kuendelea na ziara yake yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi waliopo katika mkoa huo.

Join our Newsletter