Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 20Article 572905

Habari Kuu of Saturday, 20 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Miaka 60 ya Uhuru, Mahakama Kuu ina mengi yakujivunia- Jaji Rumanyika

Sam Rumanyika,  Jaji  Mahakama Kuu ya Mwanza Sam Rumanyika, Jaji Mahakama Kuu ya Mwanza

“ Mhiili wa mahakama ikiwemo Mahakama Kuu ya Tanzania ina mengi ya kujivunia baada ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika (Tanzania).”

Hiyo ni kauli ya Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Sam Rumanyika alipozungumza na HabariLEO juu ya mambo ya msingi yaliyopatikana kwenye mhimili wa mahakama hiyo nchini.

Ushahidi wa kauli yake hiyo unadhihirishwa na ukweli kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania baada ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika kila wakati inazidi kuchanua, kung’ara na kuwa kijana muadilifu na wa kisasa zaidi. Jaji Rumanyika anasema kumbukumbu zinaonesha kuwa ikiwa na majaji watatu tangu kuanzishwa kwake takribani miaka 100 iliyopita, leo hii taifa linapoadhimisha miaka 60 ya uhuru wapo majaji zaidi ya 70 wakiwemo wanawake 23 wanaofanya kazi katika mahakama kuu iliyoanzishwa chini ya utawala wa mkoloni Muingereza.

Anasema baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1918 na kwa mujibu wa Mkataba maarufu wa Versailes uliosainiwa Juni 28 mwaka 1919 chini ya Umoja wa Mataifa (League of Nations), mchakato ulianza.

“Ujerumani ililazimishwa kumuachia Mwingereza koloni la Tanganyika hivyo sera ya Uingereza kwetu ilianza rasmi mwaka 1920, chini ya Sheria ya Uingereza ya Mamlaka ya Mambo ya Nje ya mwaka 1890, Uingereza ilitoa rasmi tamko la sheria ya kifalme iliyoitwa Tanganyika Order in Council 1920 la Julai 22, 1920 ambapo chini ya Ibara ya 17(1) ya Tamko hilo, Machi Mosi, 1921 Mahakama Kuu ilianzishwa katika koloni la Tanganyika.

Anasema Mahakama Kuu iliendelea kufanya kazi kwa kutambuliwa na tamko hilo la kifalme hadi baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Kigeni, Ralph Windhan na Jaji wa mwisho aliyeitwa Philip Georges. MAJAJI WAZAWA Jaji Rumanyika anasema mwaka 1964 majaji wawili wazawa wa kwanza waliteuliwa ambao ni Agustino Said (marehemu), ambaye baadaye aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa kwanza mzawa mwaka 1971-77 na Merk P Kimicha.

Katiba ya nchi Ibara ya 107A (1) ilikabidhi rasmi mamlaka ya utoaji haki kwa mahakama pekee ambapo pia chini ya Ibara ya 107(A) na 108 Katiba iliitambua rasmi mahakama kuu.

Imetamka: “Kutakuwa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano itakayojulikana kwa kifupi kama Mahakama Kuu, ambayo mamlaka yake yatakuwa kama ilivyoelekezwa katika Katiba hii au katika Sheria nyingine yoyote.” Anafafanua kuwa Ofisi ya Jaji Kiongozi ambaye ndiye Jaji Mfawidhi wa Masjala Kuu na Mkuu wa Mahakama Kuu nchini imeanzishwa chini ya Ibara ya 109 (1) na uteuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu unaofanywa chini ya Ibara ya 109 ya Katiba.

“Hayo yote na matokeo ya kuimarika kwa utendaji wa mhimili wa kimahakama ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika,” anasema. Anasema mwaka 1977- 2000 Jaji Francis Nyalali (marehemu) alikuwa Jaji Mkuu wa pili mzalendo kuiongoza mahakama kuu na hatimaye Mkuu wa Mahakama ya Rufani Tanzania na huo ukawa ni mwendelezo wa majaji wazawa kuiongoza mahakama kuu hadi leo hii.

UTENDAJI KAZI

Jaji Rumanyika anasema pamoja na nafasi pekee ya kikatiba ya kutoa haki, ni sharti kikatiba mahakama kufuata kanuni mbalimbali zikiwemo kutenda haki kwa wote bila ya kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi.

Pia ni sharti kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi, kutoa fidia ipasayo kwa watu wanaoathirika kutokana na makosa ya watu wengine na kwa mujibu wa sheria mahususi iliyotungwa na Bunge na kukuza na kuendeleza usuluhishi kwa wenye migogoro, mambo yamezingatiwa kwa weledi na umakini ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.

Anasema hata hivyo Sheria ya Mahakama za Mahakimu Sura ya 11, Na.2 ya 1984 ilizotangazwa kwenye Gazeti la Serikali Na.112 la Julai Mosi, 1984 iliyorekebishwa Novemba 2019, inataka kila mkoa na wilaya kuwa na mahakama, jambo hili limeendelea kufanyika kwa mafanikio.

UPATIKANAJI HAKI

Ili kuwezesha haki kupatikana na kuwafikia watu wote kwa wakati, tofauti na ile ya mahakama ya kale, Jaji Rumanyika anasema Mahakama ya Tanzania ilijiwekea mpango mkakati wa miaka mitano wa maendeleo unaohusu ujenzi na ukarabati wa majengo ya mahakama kufuatia matakwa ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025.

Kwa mujibu wake, mpango mkakati huo unatekelezwa kwa kuangalia idadi ya watu na wingi wa mashauri, maeneo mapya ya kiutawala, umbali wa wananchi kupata huduma, shughuli za kiuchumi na mazingira ya kijiografia. Anasema katika utekelezaji wa miundombinu, Mahakama ya Tanzania hivi karibuni imejenga majengo ya vituo sita jumuishi vya utoaji haki (IJCs) yanayokidhi haja na kasi ya karne ya 21 katika mikoa ya Dar es Salaam (Kinondoni na Temeke), Mwanza (Ilemela-Buswelu), Dodoma na Morogoro.

Anafafanua kuwa kwenye majengo hayo zinapatikana huduma za mahakama ya mwanzo, wilaya, hakimu mkazi, mahakama kuu na sehemu ya mahakama ya rufaa hatua ambayo anasema ni mafanikio ya utendaji kazi wa mahakama ndani ya miaka 60. “Aidha, mahakama mpya ya mwanzo ya Buswelu katika Manispaa ya Ilemela inaanzishwa ndani ya jengo hilo na hiyo ndiyo itakuwa maana halisi ya mahakama jumuishi,” anasema.

Anasema maana yake ni kwamba bila ya kutoka nje ya jengo, mfano wananchi wa Buswelu na vitongoji vyake watapata huduma ya mahakama kuanzia mahakama ya mwanzo hadi rufani. “Hata mawakili wa kujitegemea wataendesha mashauri ya wateja wao kwa gharama nafuu hivyo inatarajiwa watapunguza ada.

Ni nderemo iliyoje kwa wateja ndani ya miaka 60 ya uhuru wetu?” anahoji. Kwa upande wa Tehama, anasema mahakama haihitaji kula kiapo kuonesha kuwa matumizi yake hurahisisha na kuharakisha utoaji wa haki achilia mbali kusogeza zaidi huduma karibu na wananchi. “Tumeanzisha na tunaendesha kwa mafanikio makubwa sana, mifumo ya kielektroniki wa kusajili na kuratibu mashauri, kupitia simu yako unaweza wakati wowote ukiwa mahali popote kuona kesi gani, iko mahakama gani, mbele ya jaji au hakimu gani, imefikia hatua gani na inakuja tarehe ipi,” anasema na kuongeza kuwa mahakama pia inao tayari mfumo wa utambuzi wa mahitaji ya mahakama kwa ujumla uitwao JMAP uliotengenezwa chini ya ushauri wa Chuo Kikuu cha Ardhi.

USIKILIZAJI MASHAURI

Jaji Rumanyika anasema mahakama sasa ina mfumo mzuri wa kusikiliza mashauri kielektroniki (Video Conference and audio Teleconferencing) ambapo shauri linasikilizwa mshtakiwa au mrufani akiwa rumande au gerezani au wadaiwa wakiwa nyumbani kwao au ofisini kwa mawakili wao pamoja na walioko nje ya nchi au kokote kwenye hali ya utulivu na kimtandao.

Anasema mfumo huo uliziwezesha mahakama za hapa nchini kusikiliza na kuamua mashauri mengi mno kipindi cha janga la Covid-19 mwaka jana kiasi cha kuzishangaza nchi nyingi duniani. Katika kuepusha msongamano wa watu mahakamani, mashauri 656 kati ya mashauri 2,020 yaliyomalizika mwaka jana, yalisikilizwa kimtandao na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza pekee.

“Kwa sasa kiwango cha utendaji kazi cha kila mtumishi kinaratibiwa na kupimwa kwa ubora ki-takwimu, aidha mifumo yote hii imejengwa na inaendeshwa na watumishi wa mahakama kwa umiliki wa asilimia 100,” anasema.

Kwa upande wa mahakama inayotembea (mobile court), anasema kwa kuanzia mahakama inayo magari maalumu mawili. Moja linafanya kazi Mkoa wa Dar es Salaam na lingine mkoani Mwanza.

La Mwanza linatoa huduma katika wilaya za Nyamagana na Ilemela katika vituo vya Buhongwa, Igoma na Buswelu ambako kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika huko ndiko kuna idadi kubwa ya wananchi. Anaishukuru serikali, viongozi na watendaji mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania kwa kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya mhimili huo na kutoa haki kwa wananchi.