Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 13Article 551290

Habari za Afya of Friday, 13 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mikakati ya Serikali kudhibiti maambukizi ya TB/ UKIMWI migodini

Virusi vya Ukimwi Virusi vya Ukimwi

SERIKALI imeandaa Mpango Mkakati wa Usimamizi wa Masuala ya Ukimwi (VVU) na Kifua Kuu (TB) wenye lengo la kusaidia upatikanaji wa taarifa na udhibiti wa maambukiki ya magonjwa hayo katika maeneo ya migodini.

Mpango huo umeandaliwa na Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Hayo yalisemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Issa Nchasi wakati akiwasilisha taarifa kuhusu hali ya maambukizi ya VVU na TB katika maeneo ya migodini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Dawa za Kulevya.

Alisema mpango mkakati huo unalenga kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za maambukizi ya magonjwa hayo katika sekta ya madini na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha 2021/2022.

Amesema wa sasa Tume ya Madini kupitia Idara ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kwa kushirikiana na waganga wakuu wa wilaya inaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo juu ya masuala mbalimbali ikiwamo maambukizi ya VVU na TB.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema mazingira ya uchimbaji mdogo kwenye maeneo yenye leseni na yenye milipuko ya madini kwa kiasi kikubwa yanakosa miundombinu wezeshi ya kulinda afya na usalama wa wachimbaji, hivyo mkakati huo utapunguza maambukizi hayo kwa kiasi kikubwa.

“Tabia ya wachimbaji kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine kufuatana na uzalishaji wa madini inachangia ongezeko la maambukizi ya VVU na TB, utekelezaji wa mkakati huu utapunguza maambukizi kwa kiasi kikubwa.”

“Niipongeze kamati kwa ushauri wao makini wanaotupatia katika kuhakikisha sekta ya madini inasimamia afya za wadau wanaojishughulisha na shughuli za uchimbaji madini kwenye maeneo mbalimbali nchini,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na magonjwa yasiyoambukiza, Dk Alice Kaijage aliipongeza Wizara ya Madini kwa kuandaa mpango mkakati huo kwa ajili ya kupunguza maambukizi ya VVU na TB katika maeneo ya migodi pamoja na wachimbaji wadogo.

“Kamati inaielekeza Wizara ya Madini kuyatekeleza yote yaliyomo kwenye mpango mkakati huo ili kutoa matokeo mazuri kwa wachimbaji. Pia endeleeni kutoa elimu kwenye maeneo yanayozunguka migodi kuhusu maambukizi ya VVU na TB na kuhakikisha Tacaids (Tume ya Kudhibiti Ukimwi) inawafikia wachimbaji wadogo,” alisema.

Ofisa wa Tacaids, Nyangusi Laiser amesema elimu imeendelea kutolewa kupitia dawati maalumu katika maeneo ya migodi na wachimbaji wadogo ili waweze kujikinga na maambukizi ya VVU na TB.

“Tunaendelea kutoa elimu kupitia dawati maalumu na tunashirikiana kwa karibu na Wizara ya Madini ili kuhakikisha tunawafikia wachimbaji wengi zaidi tukilenga kutoa mikopo na kondomu ili kusaidia,” alisema.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi imepanga kutembelea migodi hapa nchini ili kujionea shughuli mbalimbali katika maeneo hayo ili kutoa elimu kuhusu VVU na Kifua Kikuu.