Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 23Article 553153

Habari Kuu of Monday, 23 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mikoa 13 itakayofanyiwa majaribio ya Sensa

Mikoa 13 itakayofanyiwa majaribio ya Sensa Mikoa 13 itakayofanyiwa majaribio ya Sensa

KAMATI ya Sensa ya Taifa kwa kushirikiana na Ofi si ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema majaribio ya sensa ya taifa ya watu na makazi Septemba mwaka huu inatarajiwa kushirikisha mikoa 13.

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii NBS, Lucy Minja alisema, kwa mara ya kwanza sensa hiyo itahusisha pia ukusanyaji taarifa za majengo yote nchini na anuani za makazi.

Minja alitaja mikoa itakayohusika katika sensa ya majaribio kuwa ni Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza, Arusha, Manyara, Singida, Dodoma, Njombe, Pwani, Mtwara, Morogoro na Dar es Salaam.

Alisema mikoa hiyo imechaguliwa kwa kuzingatia vigezo kikiwemo cha idadi kubwa ya watu na ugumu wa kufika katika baadhi ya maeneo yake.

Minja alitoa taarifa hiyo mjini Iringa wakati Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga akifungua mafunzo ya sensa kwa makarani 212 wataoshiriki kukusanya taarifa katika sensa hiyo ya majaribio. “Katika majaribio hayo ya sensa tutakuwa na madodoso makubwa manne.

Dodoso la kwanza ni la jamii litakalotumika kukusanya taarifa za huduma mbalimbali za jamii katika maeneo ya kuhesabia na dodoso la pili litatumika kuuliza taarifa mbalimbali katika ngazi ya kaya,”alisema.

Minja alisema dodoso lingine kuwa ni la majengo litakalotumika kukusanya taarifa za majengo na la nne ni la anwani za makazi ya watu wote nchini, wawe raia au wasio na uraia.

Alisema kabla ya kufanya sensa ya watu na makazi, ni kawaida kufanya sensa ya majaribio mwaka mmoja kabla ili kupima utayari wa serikali katika kufanikisha kazi hiyo zikiwemo nyezo zitakazotumika yakiwemo madodoso, miongozo na matumizi ya tekenolojia ya vishikwambi.

Minja alisema Septemba 8 hadi 10 makarani watasambazwa katika maeneo yaliyochaguliwa katika mikoa hiyo kukusanya taarifa za huduma za jamii.

Alisema Septemba 11 hadi 13 watahoji ngazi ya kaya, septemba 14 hadi 16 watakusanya taarifa za majengo na Septemba 17 hadi 19 itakuwa ni kukusanya taarifa za anwani za makazi.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anna Makinda alisema sensa ni muhimu kwa taifa kwa kuwa husaidia kufahamu mahitaji ya taifa kwa kila sekta.

“Sensa hii ya majaribio ni maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Agosti 2022. Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum.,” alisema Makinda.

Alisema Sensa ya Watu na Makazi ni kazi ya kitaifa inayofanyika kila baada ya miaka 10 na kwamba sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 2012.