Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 12Article 551158

Habari za Afya of Thursday, 12 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mikoa yote kupokea chanjo ifikapo Agosti 15

Mikoa yote kupokea chanjo ifikapo Agosti 15 Mikoa yote kupokea chanjo ifikapo Agosti 15

WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima amesema usambazaji wa chanjo ya corona nchi nzima utaanza kufanywa Agosti,2 mwaka huu na hadi ifikapo Agosti 15, mikoa yote itakuwa imeshapokea kiasi cha chanjo kwa ajili ya kuwachanja bure Watanzania walio tayari.

Aidha, saa chache baada ya Rais Samia Suluhu kuzindua chanjo ya virusi vya corona (Covid-19), Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam, mjadala mkubwa uliibuka kwenye mitandao kuhusu mtaalamu wa afya kumchoma Rais chanjo hiyo bila kuvaa glovu, imeelezwa kuwa kwenye utoaji chanjo hakuna mwingiliano unaoweza kusababisha majimaji damu.

Dk Gwajima akielezea utaratibu wa jinsi serikali ilivyojipanga kusambaza chanjo hiyo kwenye mikoa yote, alisema kuanzia Agosti, 2, chanjo itaanza kusambazwa na Mkoa wa Dar es Salaam utapata mapema zaidi ya mikoa mingine.

Alisema chanjo hiyo ya serikali itatolewa bure kwenye vituo vitakavyotajwa na makundi ya kipaumbele yatazingatiwa na kuwataka wananchi walio tayari kujitokeza pindi watakapotaarifiwa chanjo kufika kwenye mikoa yao.

“Tulipokea chanjo ya Johnson & Johnson milioni moja na kidogo hivi, tumeifanyia uchunguzi wa kisayansi kujiridhisha usalama wake na tumeridhia, sasa tunatamani Watanzania wengi wapate wale, ila iko kidogo, tunaendelea kuangalia utaratibu wa kuingiza nyingine ili watu wote wanaotaka wapaete,” alisema Dk Gwajima.

Alisema matagemeo yao ni kuwa hadi Agosti 15 chanjo hiyo iwe imeshafika mikoa yote na wahitaji waanze kupata kwa utaratibu utakaowekwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ambaye alichoma chanjo hiyo jana kwenye uzinduzi huo uliofanywa Viwanja vya Ikulu, alisema baada ya Rais kuzindua kwa kuonesha mfano, imekata propaganda zote za uongo.

“Mimi nimechanjwa kwa hiari yangu, Rais kakata propaganda zote za uongo kuhusu chanjo. Niwaambie tu watu wa Dar es Salaam kuwa tunaweka utaratibu kwa kutoa chanjo kwa wananchi na tutawaambia vituo vitakavyotoa chanjo hiyo,” alisema Makalla.

Aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata chanjo ili kuwa na kinga na kupunguza madhara ya corona .

Viongozi wa dini ambao nao walijitokeza kuchanjwa ni pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo ambaye alisema anaunga mkono serikali kwenye mapambano ya corona na kuwataka waumini wa KKKT na wananchi wote kujitokeza kupata chanjo hiyo.

“Nimechoma kwa hiari yangu, niwasihi waumini na Watanzania tusikubali kupotoshwa na baadhi ya viongozi wa dini, chanjo ni salama, wajibu wetu ni kuhamasisha watu wachome, tujilinde,” alisema Dk Shoo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Yuda Thadeus Ruwa'ichi ambaye naye alikuwa miongoni mwa viongozi wa dini waliopata chanjo ya corona jana, alisema chanjo ni faraja kwa wananchi na kuwataka waumini wa Kanisa Katoliki kuridhia chanjo hiyo na kujitokeza kuchanjwa.

“Sisi tumebahatika kuwa wa kwanza kuchanjwa siku ya uzinduzi, nimechanjwa kwa hiari yangu na chanjo ni salama, nawasihi waumini wenzangu na wananchi tusipoteze nafasi hii,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.

Mufti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir aliyepata chanjo hiyo, alisema ni jambo zuri na amedhihiri kwa hiari yake na kuwataka waumini wa Kiislamu na wananchi kwa ujumla kuchanja na kuondoa wasiwasi.

“Mimi nimepata chanjo, nahimiza Waislamu tuchanje, sina wasiwasi siwezi kuwaambia Waislamu jambo litakalohatarisha maisha yao, hii chanjo ni salama nendeni mkachanjwe, tukijinge na corona,” alisema Mufti Zubeir.

Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima baada ya kupata chanjo, aliishukuru serikali kwa hatua hiyo njema na kuhakiki chanjo hiyo, na kuwataka wananchi kujitokeza kuchanjwa.

“Ninaomba waumini wetu wajitokeze kupata chanjo, tuoneshe mfano, tuchanje tutokomeze corona,” alisisitiza.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alichanjwa na kueleza kwamba alikuwa akiisubiri kwa hamu kwa sababu yeye na askari wenzake ni moja ya makundi yaliyo hatarini kupata maambukizi ya corona kutokana utendaji kazi wao.

Kamanda Muliro alisema askari ni mtu anayetakiwa kuwa na afya imara, ikiwa afya yake imetetereka kufanya kazi ipasavyo na umakini unaondoka na kuwa corona ni ugonjwa mbaya ambao hauna budi kupata chanjo ili kujikinga nao.

“Tumepokea kwa furaha kubwa, kwa kuchanjwa chanjo hii nimejiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kulinda eneo langu, nashauri wengine wanaostahili kuchanjwa wakachanjwe,” alisema Kamanda Muliro.

Akizungumzia suala la kuvaa glovu kwa wataalamu wa afya, daktari Sabrina Murji wa Hospitali ya Hans Mganya, Dar es Salaam alifafanua kuwa utoaji wa chanjo huwa ni wa misuli au chini ya ngozi hivyo hauna mara nyingi mwingiliano wa majimaji au damu kati ya anayechomwa na anayechoma.

“Hakuna mwingiliano labda tu kati ya anayechoma na anayechomwa au ana vidonda, hapo lazima avae glavu wakati wa kutoa chanjo, na cha msingi kama hakuna kidonda inatosha kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono kabla ya kumhudumia mtu anayefuata, inatosha,”alisema Dk Murji.

Wizara ya Afya pia ilifafanua katika mitandao yake ya kijamii kuwa kwa mujibu wa mwongozo wa Covid-19, glovu hazishauriwa kuvaliwa wakati wa kuchoma chanjo yoyote na pia kwa chanjo ya Covid-19.

“Hivyo tunapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa mhudumu aliyewachoma chanjo Mheshimiwa Rais na viongozi wengine alikuwa sahihi kutovaa gloves,” ilieleza Wizara ya Afya.

Viongozi wengine waliopata fursa ya kuchanjwa kwa hiari yao jana ni Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na mkewe Tunu Pinda na mama yake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro.

Pia Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi, Hussein Katanga, Kamishna wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala, viongozi wa dini, wakuu wa wilaya mkoani Dar es Salaam, viongozi wa vyama vya siasa na wengine.

Mratibu wa Chanjo Ukanda wa Afrika wa WHO,Dk Phionah Atuhebwe alisema maambukizi ya virusi vya corona aina ya Delta barani Afrika yamezikumba nchi 29 hadi sasa.

Aidha alisema dozi milioni 12 za chanjo ya corna zimeshawasili barani Afrika mwezi huu wa Julai na kuwa mategemeo yao ni kuwa idadi hiyo itaongezeka zaidi mwezi ujao wa Agosti.

Dk Atuhebwe alisema bara la Afrika hadi sasa limeshapokea chanjo milioni 91 na kuwa watu milioni 24 sawa na asilimia 1.7 ya idadi ya watu barani humo wameshachanjwa.

Alisema Bara la Afrika linahitaji chanjo zaidi ya milioni 183 ili kuchonja asilimia 10 ya watu wake ifikapo mwishoni mwa Septemba mwaka huu na kuwa ili kufikia lengo ya kuchanja asilimia 30 ya watu barani humo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, zinatakiwa chanjo milioni 729.

Lengo la mpango wa COVAX ni kusambaza chanjo milioni 520 barani Afrika ifikapo mwishoni mwa mwaka 2021.

Alisema tayari maandalizi ya kusambaza chanjo hiyo yamekamilika na zitakuwa zimewasili kwenye mataifa hayo ifikapo mwisho wa Septemba ,2021.

Aidha alisema Umoja wa Ulaya nao umepanga kupokea chanjo milioni 16 kati ya chanjo milioni 400 za aina ya Janssen ifikapo mwishoni mwa Septemba mwaka huu.