Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 21Article 558877

Habari za Mikoani of Tuesday, 21 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Milioni 480 kujenga Bwawa la mifugo Lindi

Milioni 480 kujenga Bwawa la mifugo Lindi Milioni 480 kujenga Bwawa la mifugo Lindi

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo lenye thamani ya shilingi milioni 480 katika Kijiji cha Kimambi, wilayani Liwale, Mkoani Lindi.

Ulega, ameyasema hayo wakati wa ziara yake wilaya ya Liwale, mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza kero za wafugaji na Wakulima ili kuzitatua.

"Rais Samia Suluhu, anakwenda kuwajengea bwawa lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 hapa Kimambi, ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kuwaondosha katika migogoro," amesema Ulega.

Aidha, amesema kuwa Rais Samia Suluhu, amewapa pia majosho mawili katika kijiji cha Kimambi na kijiji cha Luwele.

"Sasa kwa sababu huku mifugo imekuwa mingi sana, mimi nakuongezeeni Josho lingine hapa ili mifugo mingi iweze kuogeshwa ," aliongeza Ulega

Naye, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita,Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea pesa hizo huku akisema kuwa bwawa hilo likikamilika hawatarajii tena kuona migogoro katika vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya wafugaji wilayani humo.