Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 04Article 540913

Diasporian News of Friday, 4 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Miradi miwili kuondoa uhaba wa maji Zanzibar

Miradi miwili kuondoa  uhaba wa maji Zanzibar Miradi miwili kuondoa uhaba wa maji Zanzibar

MIRADI miwili inayoelnga upatikanaji wa maji safi na salama inayotekelezwa na serikali ya India kupitia Benki ya Exim kwa kiasi kikubwa itasaidia kuondoa tatizo la uhaba wa maji Zanzibar.

Akijibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Suleiman Masoud Mohamed alisema miradi hiyo ni pamoja na wa uhuishaji na uimarishaji wa miundombinu ya maji utakaogharimu dola za Marekani milioni 92.18.

Wajumbe hao wa Baraza walikuwa wakijadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021-2022.

Kuhusu mradi wa maji safi na mazingira utakaogharimu dola za Marekani milioni 35, Waziri Suleimn alisema utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwawezesha wakazi wa Mkoa wa Magharibi kupata maji safi na salama.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza miradi miwili inayogharamiwa na Benki ya Exim kutoka India ambayo ni muhimu na itasaidia upatikanaji wa maji safi na salama katika Mkoa wa Magharibi Unguja,'' alisema.

Alisema kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Salama (ZAWA) kwa sasa ni kulinda miundombinu ya maji pamoja na kujenga vyanzo hivyo kwa kuzungushiwa uzio.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano kumejitokeza tatizo la wananchi kuvamia vyanzo vya maji kwa kujenga makazi ya kudumu huku akisema maeneo ya Kiyanga yanaongoza kwa uvamizi huo.

“Tunakabiliwa na tatizo moja kubwa la uvamizi wa vyanzo vya maji safi na salama. Kwa hali hiyo, sasa visima vyote vya Mamlaka ya Maji Safi na Salama vitajengewa uzio,” alisema.

Aidha alisema serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kuchimba visima wa Ras Al Khaimah unaohusisha ujenzi wa visima pamoja na kuweka miundombinu ya usambazaji maji safi na salama katika mikoa ya Unguja na Pemba.

Alisema zaidi ya visima 30 vipo katika hatua ya mwisho ya kuwekewa umeme kwa ajili ya kuanza uzalishaji na kusambaza huduma hizo kwa wananchi.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliidhinisha Sh 98,635,237,000 kwa kazi za kawaida za wizara hiyo pamoja na maendeleo. Sh 5,862,600,000 ni kwa ajili ya kazi za kawaida na Sh 92,772,637,000 kwa miradi ya maendeleo.

Join our Newsletter