Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 15Article 542791

Habari Kuu of Tuesday, 15 June 2021

Chanzo: ippmedia.com

Mjadala kodi za majengo moto

Mjadala kodi za majengo moto Mjadala kodi za majengo moto

Wakichangia bajeti ya serikali iliyowasilishwa Alhamisi iliyopita pamoja na taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Fedha iliyowasilishwa jana bungeni, wabunge walisema suala hilo lina sintofahamu kati ya wapangaji na wamiliki wa majengo.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Juliana Shonza, alisema kodi ya majengo ilikuwapo miaka mingi, lakini matatizo yake ni wananchi walikuwa hawalipi akiwamo yeye.

“Sijawahi kulipa kodi ya majengo na ni kutokana na usumbufu ambao ukifikiria utoke ukapange foleni TRA, lakini serikali imekuja na ubunifu wa kukusanya kodi hii na imetumia akili ikusanywe kwa akili kuliko kutumia mabavu,” alisema.

Shonza alisema yapo matatizo yaliyopo kwenye kodi hiyo,  na kwamba wanatambua serikali imekuja na jambo jema na ubunifu mzuri, lakini ni lazima isimamie ili katika utekelezaji wa agizo hilo kusiibuke sintofahamu.

“Sheria ya majengo ya awali inasema kabisa kwamba suala la kulipa kodi ya majengo ni la mwenye nyumba na siyo suala la mpangaji.

“Kwa hiyo kwenye agizo hili nimwombe sana mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, atakaposimama hapa atuambie serikali imejipangaje, ina mkakati gani ili kuondoa sintofahamu kati ya mwenye nyumba na mpangaji.

“Ni kweli mmiliki wa nyumba ni mwenye nyumba kwa kuwa kodi inakatwa kwenye Luku maana naye atakayekatwa ni mpangaji siyo mwenye nyumba, naomba serikali ije na utaratibu mzuri kuhusiana na kodi hii.”

Mbunge wa Vunjo, Dk. Charles Kimei, alihoji kodi ya majengo ambayo inatozwa kwa njia ya Luku atakayetozwa ni mwenye jengo au mpangaji.

“Sasa hapo unamtoza mwenye jengo au mpangaji, tuangalie namna nzuri ya kukusanya mapato haya,” alisema.

Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, alisema alisema wazo hilo lina ubunifu ndani yake na kutoa angalizo kwamba yupo mtu ana nyumba ya ghorofa kwa maana vyumba viwili juu na viwili chini na analipa Sh. 5,000 na kuhoji mwenye vyumba vitano chini kwa nini alipishwe Sh. 1,000.

“Kuna mtu ana vyumba saba ana wapangaji watatu na kila mmoja ana Luku yake atalipa Sh. 3,000 sasa kwa nini huyu analipishwa Sh. 3,000 na mwingine Sh. 1,000 na ni vyumba saba vile vile.

“Kuna mtu ni mstaafu kama alivyosema mwenyekiti wa kamati kwa nini huyu anapewa adhabu hiyo, suala la msingi kuna watu wapo tayari kulipa hawajapewa umeme.

“Ninapendekeza serikali iongeze fedha kwenye Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kusudi wanaotaka umeme wapewe na muwekeze kwenye mfumo wa Luku ikiwezekana hili suala la kusanyaji mapato kwa mfumo huu tusubiri ili huu utaratibu usije ukashindwa kama ule wa TRA katika kukusanya mapato haya,” alipendekeza.

Mbunge wa Kaliua, Aloyce Kwezi, aliiomba serikali izishauri kampuni za simu kama itawekezana angalau waachie Sh. 1,000 ziende kwenye TARURA kwa sababu barabara za vijijini ndiyo mishipa ya uchumi.

Mbunge wa Viti Maalum Neema Lugangila, alitaka pia itazamwe suala la tozo simu.

Awali, katika taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, iliyosomwa jana na Mwenyekiti wake, Sillo Baran, ikizungumzia kuhusu kodi hizo za majengo, ilisema ubunifu huo una lengo la kupanua wigo wa mapato ya serikali na kufanya ukusanyaji wa kodi kuwa rahisi.

“Uamuzi huu unaenda na Tamko la Serikali la awali la kurejesha ukusanyaji wa kodi hii kwa Serikali za Mitaa ambazo zina rasilimali watu katika ngazi zote za kukusanya kodi hii. Pamoja na ubunifu huu kuwa mzuri unakwenda kinyume na Sheria ya Kodi ya Majengo ambayo inaangalia majengo ambayo yako kwenye maeneo yanayotakiwa kulipa kodi hiyo,” ilisema.

Taarifa hiyo ya kamati ilisema mapendekezo hayo yanachukulia nyumba zote zenye umeme hata zile ambazo ziko vijijini lakini hazipo kwenye maeneo ambayo kwa mujibu wa sheria hazina sifa ya kutozwa kodi.

Kamati hiyo ilisema mapendekezo hayo hayatoi msamaha kwa taasisi za umma na majengo mengine ya umma ambayo yanatumia umeme lakini kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Majengo yamesamehewa kodi hiyo.

“Kuweka kiwango mfano kwa nyumba zilizoko mjini na vijijini ni kuwaumiza wananchi ambao wanaishi vijijini. Kamati inaishauri serikali kwamba ubunifu huu uende sambamba na kufanya uthamini wa nyumba na kutumia Luku kama namba ya mlipa kodi na kila Luku itozwe kulingana na nyumba ambayo Luku hiyo ipo,” alisema.