Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 26Article 553867

Habari Kuu of Thursday, 26 August 2021

Chanzo: Habarileo

Mkuu wa Trafiki ametaja sababu za kushindwa kusimamia "Level Seat" kwenye mabasi

Abiria kwenye mabasi Abiria kwenye mabasi

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limesema changamoto zilizopo katika kudhibiti kiwango cha abiria katika vyombo vya usafiri maeneo ya mijini ni wingi wa abiria na uchache wa vyombo hivyo.

Akizungumza wanahabari Agosti 25, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Willbroad Mtafungwa, amesema hata hivyo wanaendelea kutoa elimu kwa wasafiri ili kujikinga na mlipuko wa wimbi la tatu virusi vya Corona.

“Kisheria idadi ya watu inapaswa kudhibitiwa na wenye magari sisi tunachukua hatua na ndio maana magari ya mikoani hayajazi watu.

Kuhusu mijini tumeweka askari vituo vya daladala kuhakikisha madereva, makondakta na abiria wanavaa barakoa.”

“Changamoto zinakuja nyakati za asubuhi na jioni watu wanakuwa wengi wanaohitaji usafiri lakini magari yanayotoa huduma hayatoshi, hivyo tutakapochukua hatua watu wengi watabaki vituoni,” amesema Mtafungwa.

Amesema jitihada zao kubwa ni kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo, ikibidi wachukue vyombo mbadala vya usafiri ili kujikinga.

“Tunaelekeza nguvu kubwa kwenye elimu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine, lakini pia tunashauri mamlaka husika kuongeza vyombo vya usafiri wa abiria mijini,” amesema.

Mtafungwa amesema kikosi hicho kinatoa elimu kwa askari wao ili kujikinga na maambukizi hayo kwa kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara.

“Vikosi vyetu vya usalama tumewaelimisha na wakaelewa hata barabarani ukipita utakuta askari wamevaa barakoa na hatua zote za kiafya zinafuatwa.”

“Lakini licha ya elimu hiyo pia tumewaagiza kuhakikisha watu wanaopanda katika vyombo vya usafiri wanavaa barakoa na kunawa mikono,” amesema