Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 04Article 540919

Uhalifu & Adhabu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mkuu wa shule jela miaka 30 kwa kumuua mumewe

Mkuu wa shule jela miaka 30 kwa kumuua mumewe Mkuu wa shule jela miaka 30 kwa kumuua mumewe

ALIYEKUWA Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Icaciri, Jane Muthoni amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mumewe, Solomon Mwangi.

Jaji wa Mahakama Kuu Kenya, Joel Ngugi jana alimhukumu Jane na kubainisha kuwa mara kadhaa alipanga kumuua mumewe.

Hadi wakati anauawa Novemba 6, 2016 Mwangi alikuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Kiiru na wakati huo Muthoni alikuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Icaciri iliyopo mjini Kiambu nchini Kenya.

Jaji Ngugi alisema Mahakama imethibitisha kuwa Muthoni alikodi watu wamuue mumewe akimtuhumu kuwa alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine.

Mshitakiwa mwingine kwenye kesi hiyo, Isaac Ng’ang’a, alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kuthibitika kuwa alishirikiana na Muthoni kumuua Mwangi.

Aprili 22, mwaka huu Muthoni na Ng’ang’a walikutwa na hatia ya kumuua Mwangi.

Kwa mujibu wa mahakama, Muthoni alikuwa kiongozi mkuu wa mpango wa kumuua mumewe, lakini hakuhusika kwenye kitendo cha kumuua.

Mahakama jana ilielezwa kuwa, ushahidi ulithibitisha kuwa, kwa miezi kadhaa, Muthoni na Ng’ang’a walishirikiana na Patrick Njiru na Joseph Kariuki kupanga njama za kumuua Mwangi.

Kwa mujibu wa Jaji Ngugi, Njiru ndiye aliyemtafutia Muthoni watu wa kumuua mumewe. Mahakama ilielezwa kuwa, Mwangi aliuawa kwa kupigwa na kitu kichwani na kunyongwa kwa kamba.

Kwa mujibu wa Jaji Ngugi, mahakama imethibitisha kuwa Muthoni ndiye aliyempeleka Mwangi na kamba kwa wauaji.

Kariuki alikiri mahakamani na alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela. Kariuki alikuwa shahidi wa upande wa mashitaka.

Jaji Ngugi alisema, kabla ya mauaji, Muthoni alimlevya muwewe kwa dawa za mifugo ya ‘xylazine’ ili kumdhoofisha na akampeleka kwa wauaji.

Alisema ripoti ya uchunguzi ya hospitali ilionesha kuwa, Mwangi alipoteza maisha kwa kunyongwa na pia alikuwa na majeraha kichwani na miguuni.

Wakati wa utetezi, Muthoni aliieleza mahakama kuwa, aliamua kutumia dawa ya mifugo kwa kuwa awali alitumia dawa wanazotumia wasichana wanaojiuza kuwaibia wateja, lakini ikashindikana kufanisha mauaji hayo.

Awali, mashahidi waliieleza mahakama kuwa, Muthoni alikuwa akimtuhumu mumewe kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na wakala wa fedha kwa simu za mkononi.

Mwanamke aliyetuhumiwa na Muthoni aliionesha mahakama ujumbe mfupi aliokuwa akitumiwa na mke wa Mwangi kumtisha mara kadhaa.

Join our Newsletter