Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 20Article 572908

Habari Kuu of Saturday, 20 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Moto mkali wateketeza Hoteli nne Kusini Unguja

Moto mkali wateketeza Hoteli nne Kusini Unguja Moto mkali wateketeza Hoteli nne Kusini Unguja

Moto ulioanzia jikoni katika hoteli ya Villa de Coco iliyopo Jambiani, Zanzibar umeteketeza hoteli tatu na kuunguza vyumba vingine sita vya hoteli jirani ya nne, kutokana na upepo mkali wa baharini na zana chache za kuzimia moto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Suleiman Hassan amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema hakuna mtu yeyote aliyedhurika wakiwemo wageni wa hoteli hiyo pamoja na wamiliki wa hoteli.

"Tunafahamu tukio hilo. Polisi na Kikosi cha zimamoto walifika eneo hilo mwendo wa saa kumi na moja jioni na walifanikiwa kuudhibiti moto huo mwendo wa saa 2:30 usiku," Hassan aliambia Daily News Digital kwa njia ya simu.

Alieleza kuwa polisi na kikosi cha zimamoto bado wanachunguza chanzo cha moto huo. Polisi walidokeza kuwa ilikuwa ngumu zaidi kuudhibiti moto huo kwa kuwa hoteli nyingi zimejengwa kwa makuti.

Taarifa za awali zilidai kuwa hoteli tano, Villa de Coco, Sharazad, Spice Island, Fun Beach na Cobe zote ziliteketea. Lakini Polisi wamesema ni hoteli nne pekee ndizo zilizoathirika huku tatu zikiteketezwa kabisa kwa moto.

Kamanda wa Polisi amesema moto huo ulisambaa kutoka jikola Villa de Coco, hadi Cobe, Fun Beach, na kuunguza vyumba sita katika hoteli ya Spice Island. "Ilikuwa rahisi kuunguza hoteli kutokana na upepo wa baharini. Hoteli zote zipo eneo moja na pia, kunauwezekano vifaa vya kuzimia moto vilikuwa vya kawaida sana,” alisema.

Mwenyekiti wa Shehia ya Jambiani Kibigija, Sinatama Makame Haji alisema moto ulianza majira ya saa 10 jioni na hadi saa 5:30 usiku moto ulikuwa unaendelea kuwaka.

Alidai polisi pamoja na kikosi cha zimamoto wameweza kudhibiti moto huo kwa asilimia 40 pekee.

"Sababu ya moto huo bado haijajulikana," alisema nakuongeza “moto huo bado haujadhibitiwa.”

Mkuu wa Wilaya na Mkoa walitembelea eneo hilo.

Haji alimwambia mwandishi kuwa magari mawili pia yaliteketea kwa moto huo.