Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 25Article 553525

Habari Kuu of Wednesday, 25 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mpango aagiza mapadre walindwe dhidi ya corona

Mpango aagiza mapadre walindwe dhidi ya corona Mpango aagiza mapadre walindwe dhidi ya corona

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango amewahimiza waumini wawalinde mapadre na watawa ili wasiambukizwe virusi vya corona.

Alitoa rai hiyo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuuaga mwili wa Padre Paul Haule aliyekuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Petro Osterbay jijini Dar es Salaam.

Alitoa salamu za pole za Rais Samia na kusema serikali imeguswa na msiba huo kwani Padre Haule alikuwa akihubiri amani, alikuwa mpole na mnyenyekevu.

Padre Haule alikuwa Mkurugenzi wa vyombo vya habari vya Tumaini vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki nchini.

Mke wa Dk Mpango, Mbonimpawe Mpango alishiriki ibada hiyo.

Katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro juzi, Dk Mpango aliwahimiza viongozi wa dini na waumini wavae barakoa wakati wote wanapokuwa kwenye ibada na katika maombezi yanayofanyika hasa kwa wagonjwa.

Aliwataka viongozi wa dini waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa hatari wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Dk Mpango alisema, kanisa limempoteza padre aliyekuwa mvumilivu na akaomba waumini waendelee kumuombea marehemu apumzike kwa amani.

Alisema, Padre Haule alikuwa muungwana na mwenye nidhamu hata alipokuwa Paroko na kushushwa kuwa Paroko Msaidizi hakukata tamaa alifanya kazi kwa upendo.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thadaeus Ruwa’ichi jana alisema watazingatia ushauri wa Dk Mpango ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Aliwataka mapadre wote wa kanisa hilo waende kuchanjwa chanjo ya corona ili wawe salama na wahudumie jamii wakiwa salama.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi pia alihimiza wananchi wakachanjwe na wapuuze maneno kuwa chanjo hiyo si salama kwani wanahatarisha maisha yao.

Alisema, kwa kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Fransic amechanja na yeye (Askofu Mkuu Ruwa’ichi) amechanja, hakuna haja ya kuiogopa chanjo hiyo.

"Labda niulize mapadre wangapi mmechanja hadi sasa, naomba msingoje hadi yawafike, nendeni kuchanja sasa. Corona haina mjomba wala shemeji, mkachanje, kwani inaondoa uhai," alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.