Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540385

Habari Kuu of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mpango awabana waagizaji mbegu za mazao

Mpango awabana waagizaji mbegu za mazao Mpango awabana waagizaji mbegu za mazao

MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango ameziagiza kampuni zote zinazoagiza mbegu za mazao kutoka nje ya nchi kuanza kuzalisha hapa nchini, na kuitaka Wizara ya Kilimo kujipanga kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo.

Aidha, amelitaka Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kujizatiti zaidi katika uzalishaji wa mbegu bora huku akiwataka wakuu wa taasisi hizo kujipima utendaji wao katika utekelezaji huo.

Alitoa maagizo hayo wakati akiwahutubia mamia ya wananchi wa Morogoro pamoja viongozi mbalimbali alipofunga Wiki ya Maadhimisho ya Kumbukizi ya 37 tangu kifo cha Edward Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu.

Maadhimisho hayo yalifanyika Kampasi Kuu ya Edward Moringe Sokoine ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), na kuhudhuliwa na viongozi

mbalimbali wa serikali wakiwamo mawaziri wakuu wastaafu, Mizengo Pinda na Jaji Mstaafu Joseph Warioba ambaye ni Mkuu wa SUA sambamba na wahadhiri na wanafunzi wa chuo hicho.

Makamu wa Rais alisema uamuzi wa kutaka kuzalishwa kwa mbegu hizo nchini unatokana na matumizi ya teknolojia za kisasa bado ni ya kiwango kidogo, uzalishaji pamoja na usambaji wa mbegu bora bado hauridhishi.

Alisema katika kuhakikisha kampuni zinazoagiza mbegu kutoka nje zinazalisha mbegu nchini, aliiagiza Wizara ya Kilimo ijipange kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo na isisubiri mpaka atakapouliza.

Hata hivyo, aliziagiza Wizara ya Kilimo na ya Mifugo na Uvuvi kushughulikia kwa nguvu zaidi katika kupanua huduma za ugani ili ziwafikie wakulima na wafugaji wadogo wa vijijini.

“Mfumo mzima wa huduma za ugani pamoja na ufuatiliaji wa vitendea kazi unatakiwa kufanyiwa marekebisho makubwa ili kuwafikia wakulima na wafugaji wadogo maeneo ya vijijini kwa wakati ili waongeze tija,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema serikali imeweka mkazo kukuza kilimo kwa sababu sekta hiyo inatoa asilimia 70 ya ajira zote nchini, inachangia asilimia 23 ya Pato la Taifa, asilimia 30 ya mauzo ya nje na asilimia 65 ya malighafi ya viwandani.

“Kama ilivyo wakati wa uhai wa Edward Moronge Sokoine, sekta ya kilimo inabaki kuwa sekta mama katika uchumi wa taifa na chanzo cha kuaminika kwa chakula na kipato kwa Watanzania wengi,” alisema Makamu wa Rais.

Alisema pamoja na umuhimu mkubwa kilimo katika uchumi, tija katika kilimo hairidhishi akitolea mfano takwimu zilizopo zinaonesha mavuno ya mahindi nchini ni tani 1.55 kwa hekta karibu ya asilimia 15 ya mavuno ya zao hilo takribani tani 10 kwa nchi ya Marekani ambaye ndiye mzalishaji na msafirishaji mkubwa wa zao la mahindi duniani.

Alisema mwenendo huo wa tija ndogo katika sekta ya kilimo maana yake kuwa serikali, SUA na taasisi zote za mafunzo ya kilimo na utafiti bado wanayo kazi kubwa mbele ya safari ya kuinua uzalishaji, tija na masoko ya mazao ya kilimo kwani inaonekana hakujafuzu vizuri somo la hayati Sokoine.

Alisema Sokoine aliyekufa kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984, katika uhai wake alisisitiza umuhimu wa kulinda uhuru, nchi kujitosheleza kwa chakula, kuwekeza katika kilimo na ufugaji na utafiti kama msingi wa uamuzi wa kutunga na kuhuisha sera na kubadilisha maisha vijijini kuwa bora zaidi huku akichukia vitendo vya rushwa.

Mkuu wa chuo hicho, Jaji Warioba aliiomba serikali kuwekeza eneo la utafiti katika kilimo na ufugaji, akieleza kuwa utasaidia kuzifikisha kwa kutumia maofisa ugani wakulima na wafugaji walio wengi vijijini ili watumie matokeo hayo katika uzalishaji utakaoleta tija kwa kuwa asilimia kubwa wapo katika hali ya umaskini.

Join our Newsletter