Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 17Article 543226

Habari za Mikoani of Thursday, 17 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mradi wa usambazaji wa umeme ‘Peri Urban’ Dodoma wazinduliwa

Mradi  wa usambazaji wa umeme  ‘Peri Urban’ Dodoma wazinduliwa Mradi wa usambazaji wa umeme ‘Peri Urban’ Dodoma wazinduliwa

WAZIRI Nishati Dk. Medard Kalemani amezindua mradi wa usambazaji wa umeme wa ‘Peri Urban’ jijini Dodoma ambao utakamilisha usambazaji wa umeme katika maeneo yote yaliyokuwa yamesalia kufikiwa na nishati hiyo muhimu.

Katika uzinduzi huo, Waziri Kalemani amesema mradi huo umegharimu kiasi cha Sh bilioni 17.3 ambapo umelenga kusambaza umeme kwenye maeneo yote ambayo hayajafikiwa katika mitaa 222 ya jijini humo.

“Kupitia mradi huu wa umeme, mtaunganishiwa kwa Sh 27,000 kama nilivyosema awali na imani yangu ni kwamba utachochea shughuli za uchumi na kijamii hivyo niwaombe sana muitumie vizuri fursa hii,” amesema

“Kwa hivyo basi na mimi namuagiza Mkandarasi Cylex kutoka Sri Lanka kuanza utekelezaji mara moja ili baada ya mwezi mmoja na nusu nije niwashe mwenyewe hapa,” amesema Waziri Kalemani.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amewataka wananchi wote kuhakikisha wanaitumia nishati hiyo kama kichocheo cha kujiletea maendeleo na hasa kwenye kuongeza ufaulu kwa watoto wa shule ambao watapata muda mrefu wa kujisomea katika mazingira rafiki kuliko ilivyokuwa awali.

Awali, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde aliishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya usambazaji wa umeme ya Peri Urban na Densification ambayo kukamilika kwake kutaliwasha Jiji lote la Dodoma na hivyo wananchi kutumia nishati hiyo kujiletea maendeleo mbali mbali hasa katika sekta za kiuchumi.