Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 23Article 553195

Siasa of Monday, 23 August 2021

Chanzo: Nipashe

Mrema awashangaa wanaopinga chanjo corona

Mrema awashangaa wanaopinga chanjo corona Mrema awashangaa wanaopinga chanjo corona

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema, amewataka wananchi kuwapuuza baadhi ya watu wakiwamo wanasiasa wanaopinga chanjo ya corona, akidai kila mtu anawajibika kwa afya yake.

Aidha, amesema kuchanja ni sawa na polisi anapokwambia funga mkanda unapokuwa kwenye gari, anakusaidia ili ukipata ajali usipate madhara zaidi.

Akizungumza jana katika mahojiano nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam, alisema kuendelea kuwasikiliza wanaopinga chanjo hiyo ni kupoteza muda, kwani kila mtu anatakiwa kujali afya yake mwenyewe.

Alisema ameshapata chanjo na hawezi huchezea afya yake. Alihoji kuwa watu wote wakiugua corona, mitungi ya gesi ya oksijeni utapatikana wapi na kwamba watafia majumbani.

Mrema alisema siyo mara ya kwanza kwa wananchi wa Tanzania kupata chanjo, lakini inashangaza chanjo hii ya corona imekuwa na upinzani mkali sana, na cha kushangaza miongoni mwa wanaopinga ni viongozi wa kisiasa.

“Kuchanja sawa na polisi anapokwambia funga mkanda unapokuwa kwenye gari, anakusaidia ili hata ukipata ajali huwezi kuumia sana, kwa sababu mkanda utakuzuia," alisema Mrema.

Mrema alisema hofu kwamba waliochanjwa baada ya muda watakuwa mazombi, hizo ni kauli za kuwatia hofu kwani wataalamu waliobobea wa masuala ya afya wameshathibitisha kuwa chanjo hiyo ni salama.

Alisema hakuna sababu ya kuingiwa na hofu katika suala hili, kwani bahati nzuri hata Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha njia kwa kupata chanjo hiyo, ambayo inaendelea kutolewa katika nchi mbalimbali duniani.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiikosoa chanjo hiyo, hivyo kuibua malumbano na baadhi ya viongozi wa serikali.

Mpaka Agosti 14, mwaka huu idadi ya wanaume waliochanjwa ni asilimia 58.3 sawa na 121,002 na 86,389 ni wanawake sawa na asilimia 41.7.