Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 13Article 551371

Siasa of Friday, 13 August 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Msajili wa Vyama ampiga barua ya maelezo Mnyika

John Mnyika, Katibu Mkuu CHADEMA John Mnyika, Katibu Mkuu CHADEMA

Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi, amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, akimtaka kujieleza kuhusu kauli aliyotoa kwenye mkutano wake na waandishi wa habari dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Agosti 10, 2021 Mnyika alizungumza na vyombo vya habari kuhusu mahojiano ya Rais Samia na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) yaliyofanyika siku moja kabla, ambapo alisema “Rais alisema uongo au alipotoshwa na wasaidizi wake.”

Jana, Agosti 12, 2021 Mnyika aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akieleza kwamba Jaji Mutungi amemtaka awasilishe maelezo yake leo Agosti 13, 2021.

“Msajili wa vyama ameniletea barua Agosti 12, 2021 kutaka niwasilishe maelezo leo kwa niliyoyasema Agosti 10 kuwa Rais alitoa kauli za uongo kwenye mahojiano yake na BBC. Amedai kutumia maneno hayo ni lugha chafu, kashfa na kinyume na maadili"

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amekiri kuwa wamemwandikia barua Mnyika, lakini hakutaka kueleza kilichoandikwa katika barua hiyo kwa sababu ni mawasiliano ya kiofisi.

“Ni kweli tumemwandikia barua, sasa mwambie akupe hiyo barua tuliyomwandikia maana mengine anayoongea yasije yakawa hayapo,”

Alipoulizwa yaliyomo kwenye barua hiyo, Nyahoza amesema kuwa walimwandikia barua kiofisi na kiungwana ila Katibu huyo akaenda kwenye mitandao kitu ambacho sio ustaarabu.

"Yeye aliyevujisha akwambie kwa sababu sisi hatukwenda kwenye vyombo vya habari tulipomwandikia, sisi tulimwandikia kiofisi kabisa, kiungwana, kimya kimya, yeye akaenda kwenye vyombo vya habari, Twitter, kitu ambacho siyo ustaarabu.”