Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 03Article 567823

Habari Kuu of Wednesday, 3 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Msanii Vitali Maembe Adaiwa Kukamatwa na Polisi

Vitali Maembe Vitali Maembe

WAKATI taarifa za kukamatwa kwa msanii Vitali Maembe zikiendeleaa kusambaa, Jeshi la Polisi linaonekana kuwa kimya huku likisema linafuatilia taarifa hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa baada kutafutwa kwa njia ya simu ili alitolee ufafanuzi jambo hilo, haya ndiyo yaliyojili. ”Asante kwa taarifa, tunazifuatilia” amejibu aliyepokea simu ya RPC na kusema RPC yuko kwenye kikao hivyo ameacha simu yake ofisini.

Kwa upande wake, akinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani hii leo, RPC Nyigesa amesema ameyasikia madai ya kukamatwa kwa msanii huyo hivyo anafuatilia ili kupata ukweli na kulitolea majibu.

Wakati huo huo, Zitto Kabwe ambae ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, kupitia ukurasa wake wa Twitter, amelitaka Jeshi la Polisi kumuachia msanii huyo.

"Nawataka Jeshi la Polisi Tanzania kumwachia huru mara moja ndugu Vitalis Maembe. Polisi Mkoa wa Pwani wamefanya la hovyo sana kumkamata Vitalis kutokana na kazi ya ya kisanii ya wimbo wa Kaisari. Haivumiliki na tunataka Vitalis aachiwe huru sasa hivi,” ameandika Zitto.

Ikumbukwe kwamba Vitalis Maembe hutumia mziki wake, kueleza madhila wanayoyapata watu wa kawaida, huku akijichukua yeye kuwa sauti yao na kuwasilisha hoja hizo. Ingawa kazi yake, imekuwa ikinasibishwa na uanaharakati.

Vile vile Vitalis Maembe ni miongoni mwa wasanii waliohitimu katika wa Chuo cha Sanaa Bagamoyo na kufanikiwa kupenyeza kazi zake za sanaa ndani na nje ya Tanzania.