Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 10Article 546340

Habari za Afya of Saturday, 10 July 2021

Chanzo: ippmedia.com

'Msisubirie maiti ziokotwe mitaani'

'Msisubirie maiti ziokotwe mitaani' 'Msisubirie maiti ziokotwe mitaani'

Amesema licha ya ugonjwa huo kudhibitiwa, wagonjwa wameendelea kujitokeza na kulazwa hospitalini.

Dk. Gwajima aliyasema hayo jana  katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam na kuwataka wananchi waelewe na wasingojee hali ya kuzoa maiti mtaani ndipo waanze kuchukua tahadhari.

“Kazi inayofanyika ni kufanya hali isiwe mbaya, serikali inajitahidi na Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) amekuwa akikumbusha 'jamani ndugu zangu tuchukue tahadhari', ili hali hii tunayodhani ipo hivi kwa sababu inashikiliwa kwa juhudi mbalimbali za kinga isije ikapitiliza,” alisema.

Waziri huyo alisisitiza kuwa wagonjwa wa corona wapo na wanaendelea kujitokeza na hiyo inamaanisha kwamba maambukizi yapo na siyo ya uongo.

“Ni nguvu kubwa sana inafanyika na watumishi wetu walio mstari wa mbele kuhakikisha hicho watu wanachokisubiri kitokee katika ngazi ile, kisitokee.

"Tunapotoa elimu tunamaanisha  kurahisisha mapambano kwa ushirikiano na nchi kwa kuchukua tahadhari,” alisema.

Waziri Gwajima alisema licha ya kutoa elimu hiyo, baadhi ya wananchi wanaitikia na wengine hawafanyi hivyo na kuwataka wafanye hivyo ili serikali iongeze wigo ili nchi iwe salama.

“Kwenye msongamano wapo wanaovaa barakoa na wengine hawavai, lakini wewe uliyepona, huumwi, umebeba kimelea na unakisambaza, waokoe basi wengine.

"Kuna wazee, wapo wanaoumwa magonjwa mbalimbali, tunawaokoaje? Wengi tukivaa barakoa, tutaokoa wengine,” alisema.

Gwajima alisema kuwa katika kueneza elimu, wanawatumia waganga wa mikoa na halmashauri na wakuu wa wilaya na mikoa husika.

“Tuna tiba asili ambazo hatujazitupa, zilisaidia wengi awali na sasa zinasaidia wengi, watu watumie, wale vyakula ambavyo ni vya asili ili kuongeza kinga.

"Idadi ya wagonjwa kwa sasa siwezi kueleza kwa sababu inabadilika, wanaweza wakawa mia (100) na wakashuka wakawa 50 au wamepanda mpaka 80, kwa hiyo siwezi kusema kwa sasa kwa sababu sijaichukua, lakini itoshe kusema wagonjwa wapo," alisema.

MITUNGI YA GESI

Katika hatua nyingine, wizara hiyo  imesema inatarajia kuweka mitambo 25 kwenye hospitali zote za mikoa na kanda nchini ili kukidhi uhitaji wa gesi tiba endapo kutakuwa na ongezeko la wagonjwa.

Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara hiyo, Dk. Leonard Subi, akizungumza na Nipashe jana kuhusu namna wanavyokabiliana na uhaba wa mitungi ya Oksijeni, alisema wanaendelea na jitihada za kuongeza uzalishaji nchini.

Alisema tayari wamesimika mitambo saba  katika hospitali saba nchini zenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 kila moja kwa siku.

Alisema mitambo hiyo yote inaweza kuzalisha mitungi 1,400 kwa siku ikiwa ni nyongeza ya uwezo uliokuwapo awali.

"Hivyo tumeendelea kuboresha mifumo ya mtiririko wa hewa tiba ya Oksijeni kwenye baadhi ya hospitali kwa kujenga mifumo hiyo ili gesi tiba inapozalishwa ipelekwe moja kwa moja kwa mgonjwa," alisema.

Aliwataka wananchi kuchukua hatua zote za kinga na kuzingatia miongozo yote iliyotolewa na wizara ili kuepuka kupata ugonjwa huo.

"Kwa kuzingatia ipasavyo tutakata mnyororo wa uambukizo wa ugonjwa huo, hivyo kujinusuru kuingia kwenye matumizi ya gesi tiba ya Oksijeni," alisisitiza Dk. Subi.

*Imeandikwa na Romana Mallya na Mary Geofrey