Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 23Article 559375

Habari za Afya of Thursday, 23 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mtaji, faida sekta ya bima waongezeka 1.6%

Mtaji, faida sekta ya bima waongezeka 1.6% Mtaji, faida sekta ya bima waongezeka 1.6%

MAMLAKA ya Usimamizi wa Shughuli za Bima Nchini (TIRA), imebainisha kuwa faida na mtaji katika sekta ya bima umeongezeka kwa asilimia 1.6 kwa kipindi kilichoishia Desemba mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2019.

Kamishna wa Bima, Dk Mussa Juma, aliyasema hayo hivi karibuni alipozungumza na HabariLEO kuhusu hali na maendeleo ya bima nchini.

Alisema kwa kipindi cha mwaka wa fedha kuanzia 2016 hadi 2018, soko la bima kwa ujumla lilitengeneza hasara badala ya faida lakini mwaka 2019/2020 likaanza kutengeneza faida.

Alisema kwa mwaka huo wa 2020 faida na mtaji katika sekta hiyo ya bima ilikuwa ni Sh milioni 827.8 wakati mwaka 2019 ilikuwa ni Sh milioni 814.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.6.

Alitaja maeneo ya biashara ya bima yaliyofanya vizuri katika kipindi hicho kuwa ni usafiri wa anga, bahari, ajali na moto.

Dk Juma alitaja wadau wakuu wa biashara hiyo waliosajiliwa na mamlaka hiyo hadi kufikia Septemba 16 mwaka huu, kuwa ni wakala wa bima 923, kampuni za bima 29, kampuni mbili za bima mtawanyo, benki zinazotoa huduma ya bima 19 na madalali bima mtawanyo wanne.

Wengine ni wathaminishaji na wakaguzi wa bima 52, madalali wa bima 70, kampuni za takwimu za bima nne na watafiti binafsi katika masuala ya bima wawili.

Hata hivyo, kamishna huyo wa bima alisema pamoja na sekta hiyo kufanya vizuri, bado mchango wake katika pato la taifa uko chini ambao ni chini ya asilimia nne.

Katika Mpango wa tatu wa Maendeleo wa miaka mitano, ulibainisha hali ya sasa ya bima nchini, ambapo takwimu zinaonesha mchango wa bima katika pato la taifa ni asilimia 0.7, lakini malengo ni kufikia asilimia mbili ifikapo mwaka 2025/26 na kiwango cha ukuaji wa sekta hiyo ya bima ni asilimia 28.5 wakati malengo ni kufikia asilimia 29.1.

Mpango huo umejielekeza katika maeneo makuu matatu ambayo ni kujenga uelewa na hamasa kwa umma kuhusu faida ya bidhaa za bima; kubuni bidhaa za bima kuendana na mahitaji ya soko na mifumo ya kushughulikia madai, malipo na malalamiko ya wateja.

Mpango unaeleza hatua zitakazochukuliwa kukuza sekta hiyo kuwa ni kuhamasisha na kuendesha programu jumuishi za elimu ya bima kwa umma, kuanzisha na kuhamasisha bidhaa za bima zinazohitajika katika kuanzisha mfumo madhubuti wa kushughulikia madai, malipo na malalamiko ya wateja.