Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 15Article 547033

Habari za Mikoani of Thursday, 15 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mtaka kuwapigia debe wafugaji

Mtaka kuwapigia  debe wafugaji Mtaka kuwapigia debe wafugaji

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ameahidi kukutana na uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujadili namna ya kuwezesha wafugaji wa mkoa huo kunufaika na shamba la mifugo la serikali la Kongwa mkoani hapa.

Alisema hayo wakati akifungua mkutano wa wafugaji wa mkoa wa Dodoma, ambao katika risala yao walilalamika kukabiliwa na ukosefu wa maeneo ya kufugia na malisho.

Mtaka aliahidi kuzungumza na viongozi wa wizara hiyo ili wawapatie wakulima wa mkoa huo vitalu vya ardhi kwenye shamba hilo la mifugo lenye ukubwa wa hekta 38,000 (sawa na ekari 95,000).

Alisema ataomba wananchi hao wapatiwe ardhi katika shamba hilo kwa utaratibu wa kukodisha ili waweze kupata maeneo ya kutosha ya kuendeshea shughuli za ufugaji wa kisasa na uoteshaji malisho ya mifugo.

Akisoma risala ya wafugaji, Katibu wa Chama cha Wafugaji Mkoa wa Dodoma, Reginaldo Lubeleje alisema maeneo mengi wanayofugia yana changamoto nyingi ikiwamo migogoro ya mipaka na ukosefu wa mipango ya matumizi bora ya ardhi.

Alisema maeneo hayo yana ukosefu wa huduma muhimu kama maji na majosho ya kuogeshea mifugo na baadhi ya maeneo ya ufugaji na malisho yamekuwa yakivamiwa kwa shughuli za kilimo.

Aidha, alisema wakulima hao wana ukosefu wa elimu ya kutosha ya ufugaji bora wakati mkoani humo kuna shamba kubwa la mifugo la serikali lakini halina mchango katika kusaidia wafugaji.