Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 21Article 573100

Habari za Mikoani of Sunday, 21 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mtatiro ataka madiwani kushiriki utekelezaji miradi

Julius Mtatiro, Mkuu wa Wilaya Tunduru Julius Mtatiro, Mkuu wa Wilaya Tunduru

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro amewataka madiwani kuwa mstari wa mbele kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotokana na fedha za serikali.

Mtatiro aliyasema hayo mjini Tunduru wakati akizungumza na madiwani na baadhi ya wakuu wa idara katika semina ya kuwawezesha madiwani uelewa wa majukumu yao, kuwajengea uwezo na kufahamu kanuni mbalimbali zinazoongoza mabaraza ya madiwani. Alisema ni muhimu madiwani wakawa sehemu ya mipango ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanywa na serikali na kuwa wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kusimamia na kutekeleza miradi katika halmashauri yao.

“Mkiona kuna kitu hakiendi sawa kwenye utekelezaji wa miradi mna wajibu wa kuchukua hatua kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa juu ili lifanyiwe kazi, madiwani mna dhamana kubwa ya kufuatilia na kusimamia miradi katika halmashauri yenu,” alisema. Aidha, aliwataka kushirikiana na wananchi na watendaji kubuni na kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kuanzisha miradi ambayo itaongeza mapato, badala ya kusubiri fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Katika hatua nyingine, Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo aliwaomba madiwani kwenda kutoa elimu kuhusu umuhimu wa ulinzi na usalama kwa kuwafichua watu wanaowatilia shaka katika maeneo yao.

Ofisa Serikali za mitaa kutoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Amandus Chilumba alisema wameamua kufanya mafunzo kwa halmashauri za mkoa huo kwa lengo la kuboresha utendaji kazi kwa watumishi mbalimbali ngazi ya halmashauri wakiwemo madiwani.

Mafunzo hayo yametajwa kuwa ni muhimu kwani yataongeza uelewa katika usimamizi wa fedha, ununuzi na utawala hasa wakati huu ambao serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia fedha za Covid-19.

Diwani wa Kata ya Masonya, Said Bwanali aliipongeza serikali kwa kutoa mafunzo hayo kwani yanakwenda kuwaongezea uelewa mkubwa juu ya usimamizi wa fedha, kutambua majukumu yao na kujenga mahusiano kati ya madiwani na watumishi.

Bwabali ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, aliiomba serikali kutoa mafunzo halmashauri nyingine za Mkoa wa Ruvuma akisisitiza kuwa yatasaidia kuongeza uelewa katika kubuni vyanzo vingi na kusimamia mapato yatakayopatikana.

Diwani wa Kata ya Namakambale, Mfaume Wadali alisema mafunzo hayo yanakwenda kuongeza tija katika halmashauri yao na watakuwa na watu wenye uelewa na uwezo wa kujenga hoja katika vikao mbalimbali vya mabaraza ya madiwani. Alisema baada ya mafunzo watakwenda kufanya kazi kwa ushirikiano na kila upande kutambua majukumu yake na kuepusha malumbano yasiokuwa na faida kwa halmashauri.