Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 20Article 572902

Habari Kuu of Saturday, 20 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mtazamo wa wasomi nchini kuhusu Lugha ya Kiswahili

Mtazamo wa wasomi nchini kuhusu Lugha ya Kiswahili Mtazamo wa wasomi nchini kuhusu Lugha ya Kiswahili

HIVI karibuni Taifa la Tanzania litatimiza miaka 60 ya uhuru. Wakati tukisherehekea miaka hiyo, hatuwezi kuacha kuihusisha lugha ya Kiswahili na kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania).

Lugha hii ilitumika katika harakati za kudai uhuru hivyo kurahisisha mawasiliano na kuifanya kuwa sababu mojawapo ya Tanganyika kupata uhuru wake mapema. Kiswahili kilitumika kama zana muhimu ya mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao.

Baada ya kupata uhuru Rais wa kwanza wa Tanganyika (Tanzania), Mwalimu Julius Nyerere alitumia Kiswahili kuhutubia Bunge la kwanza mwaka 1962. Kuanzia wakati huo lugha hii ikawa lugha rasmi ya mawasiliano katika shughuli zote za serikali pamoja na kutumika kufundishia shule za msingi na kutumika kama somo katika shule za sekondari na vyuo.

Katika makala haya tutaangalia mtazamo wa baadhi ya wasomi katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Baadhi ya wasomi hapa nchini wana kasumba au mtazamo hasi kuhusu Kiswahili wakiamini kuwa hakiwezi kusonga mbele na hata kufikia kuwa lugha rasmi ambayo itaweza kufikia hadhi ya kimataifa licha ya jitihada zinazochukuliwa na serikali na wazalendo wachache katika kutanua mawanda ya kimatumizi ulimwenguni.

Kuna baadhi ambao wamediriki kusema kwamba lugha ya Kiswahili ni changa na haijitoshelezi kimsamiati pasi kutambua kwamba lugha yoyote ulimwenguni inakuwa na kufaa kimatumizi kutokana na kutumika kwake mara kwa mara na kupewa kipaumbele na watumiaji wa lugha hiyo.

Leo hii tunashuhudia kuwa serikali kwa kukithamini Kiswahili imeanzisha kozi za kusoma Kiswahili kuanzia shahada ya kwanza hadi ya uzamivu. Hii yote ni kuona kuwa tunakuwa na wasomi wabobevu katika lugha hii ambayo inazidi kukua siku hadi siku.

Ni aghalabu kukuta msomi wa ngazi ya chuo kikuu tena wa Tanzania ambayo lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa tunu za taifa akishadidia kwamba Kiswahili ni lugha yenye mashiko, baadhi yao hudiriki kusema kuwa “Kiswahili ni lugha duni haifai kutumika katika mtaala wa elimu”.

Kwa muda mrefu sasa utekelezaji wa kubadilisha sera yetu ya elimu kutumia lugha ya Kiswahili katika mfumo wetu wa elimu umebaki kuwa kitendawili na hii ni kutokana na baadhi yetu kutokuwa na uzalendo wa lugha yetu na kuamini zaidi kwenye lugha za kigeni. Niliwahi kushuhudia mwanazuoni akisema endapo lugha ya Kiswahili ikiruhusiwa kutumika katika mfumo wetu wa elimu atawahamisha watoto wake wakasome nje ya nchi.

Kauli kama hizo zinarudisha nyuma maendeleo ya lugha yetu na kufuta ndoto za kukiona Kiswahili kikitumika kwenye mfumo wetu wa elimu. Leo tunashuhudia jinsi Kiswahili kinavyopanda chati kwa kasi kitaifa na kimataifa. Hadi sasa inakadiriwa kuwa Kiswahili kina watumiaji zaidi ya milioni 200. Katika kuthibitisha kukua na kupanuka kwa Kiswahili duniani, Profesa Mshiriki na Mgoda wa Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Nyerere katika Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Aldin Mutembei katika makala yake ya “Kiswahili kama lugha ya Mawasiliano Mapana barani Afrika”, anasema ni lugha ya 10 kutumiwa duniani. Profesa Mutembei anasema katika nchi za Afrika, Kiswahili kinatumiwa na watu milioni 224.9. Hivyo inaonesha kuwa Kiswahili kinazidi kupanda chati licha ya kuonekana kuwa ni lugha duni kwa baadhi ya wasomi hapa nchini. Aidha, lugha hii inatumika katika matumizi rasmi katika taasisi na jumuiya mbalimbali za kimataifa. Kiswahili kinatumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na Bunge la Afrika Mashariki, katika mikutano ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Bunge la Afrika na katika mikutano ya nchi za Afrika (AU). Kiswahili kimekuwa kikiendelea kukua na kutumika ndani na nje ya nchi, ambapo pia kinafundishwa katika vyuo vikuu mbalimbali duniani mfano; Havard, Yale, Stanford na Princeton vya Marekani pamoja na vyuo vya Kolon, Leipzing, Bayreuth, Humbolt, Berlin na Hamburg vya Ujerumani.

Baadhi ya wasomi wetu wanasahau kwamba lugha ya wenzetu tunayotumia katika nyanja mbalimbali ni matokeo ya kuamini na kuona lugha yao ina utoshelevu, pia wanasahau kuwa lugha zote ulimwenguni zinategemeana katika kukamilishana kwake. Mfano lugha ya Kiingereza imekopa msamiati mingi kutoka kwenye lugha ya Kifaransa, Kigiriki na Kilatini.

Na hata sisi tukiamini tunaweza kukipaisha Kiswahili kwenye anga za kitaaluma na nyanja nyingine. Niliwahi kufanya mazungumzo na mwanafunzi mmoja wa fani ya sheria kutoka chuo kimojawapo hapa nchini kumueleza jitihada za serikali yetu inazochukua kufanya fani ya sheria ifundishwe kwa lugha ya Kiswahili.

Lakini aliniambia haiwezekani Kiswahili kutumika katika fani hiyo kwa kile alichokiita ugumu wa kupata istilahi muafaka za lugha ya kilatini zilizotumika kwenye fani ya sheria, msomi huyu anasahau kuwa hata Kiingereza kinachotumika kufundishia masomo ya sheria kimeazima baadhi ya istilahi kutoka lugha ya Kilatini. Wasomi wana kasumba na kuamini kuwa lugha ya Kiswahili ni ngumu na hii inajidhihirisha wanapochanganya maneno ya kiingereza katika kuzungumza wakidhani kwamba ili uonekane umesoma lazima uchanganye lugha mbili.

Kuna jitihada kubwa za lazima zinapaswa kuchukuliwa kwa baadhi ya wasomi wetu na wanafunzi wetu kufundishwa somo la uzalendo na hii itachochea kupenda na kuthamini vitu vya kwetu. Jitihada hizi zinapaswa kuchukuliwa kuanzia ngazi ya chini hadi za elimu ya juu. Hatua hii itasaidia kuondokana na ukasumba uliotawala miongoni mwa wasomi wetu. Kiswahili ni chetu Watanzania, kabla ya kuthamini lugha za nje ya mipaka ya nchi, tuanze sisi kukithamini.

Mwandishi wa makala haya ni Mfasiri kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) 0712/0767-953400