Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 29Article 540550

Habari za Afya of Saturday, 29 May 2021

Chanzo: ippmedia.com

Muhimbili yapunguza vifo vya watoto wa uangalizi maalum

Muhimbili yapunguza vifo vya watoto wa uangalizi maalum Muhimbili yapunguza vifo vya watoto wa uangalizi maalum

Watoto hao ni wale wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali wakiwamo wa nimonia, maambukizi kwenye damu na homa ya uti wa mgongo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Tumaini la Maisha, Gerald Mongella, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya PICU Duniani yaliyofanyika Hospitali ya Muhimbili.

Mongella alisema kitengo hicho ni sehemu ya kuongeza maisha yao ambapo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019, kimehudumia watoto 1,140 na kupunguza idadi ya vifo kutoka asilimia 65 hadi asilimia 36.4.

"Ukitazama idadi ya watoto waliohudumiwa na PICU unajiuliza isingekuwapo ingekuaje. Kipimo cha mafanikio ya kitengo hiki ni kwamba kabla hakijaanzishwa ilikuwa ukipita barabara za ndani za Muhimbili hukosi mama amebeba mtoto anakwenda kuhifadhiwa chumba maalum cha maiti lakini kwa sasa inaweza kupita miezi sita kutoona hili,” alisema.

Aliwakumbusha madaktari na wauguzi kuzingatia maadili kwa kufuata miongozo yao ya kazi.

Pia aliwaomba wadau waliodhamini shughuli hiyo wajitokeze kusaidia kitengo hicho ili tatizo la vitanda liweze kutatuliwa.

Daktari Bigwa wa Watoto, kitengo cha Uangalizi Maalum (ICU) hospitalini hapo, Evance Godfrey, alisema kitengo hicho huwapokea watoto wanaopata rufani kutoka hospitali mbalimbali nchini na lengo lao ni kupunguza idadi ya vifo kwa asilimia 20.

Alisema matatizo yaliyopo ni huduma ya ICU kwa watoto hazijasambaa, hawana wataalamu wa kutosha na kuomba waliopo waendelee kupewa mafunzo.

Alisema tangu kuanzishwa kwa kitengo hicho wagonjwa wengi wanaowapokea ni nimonia ni asilimia 17, maambukizi kwenye damu asilimia 16 na homa ya uti wa mgongo asilimia 15.

Mkuu wa Kitengo cha PICU, Dk. Yasser Harbesh, aliwashukuru wafanyakazi wa kitengo hicho na wadau wengine ambao wamekuwa wakijitoa kwa ajili ya kusaidia kuhudumia watoto hao.

Katika maadhimisho hayo wafanyakazi bora ni muuguzi Maimuna Yusuph na Daktari Emmanuel Masawe, ambao wote wamepatiwa zawadi maalum kama motisha ya kazi.

Muuguzi Maimuna alisema amefanya kazi hiyo kwa miaka 20 na moja ya tatizo kubwa kabla ya kuanza kitengo hicho ilikuwa ni kitendo cha kuona mtoto anayehitaji huduma ya mashine ya kupumulia au nyingine na kukosa.

Join our Newsletter