Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 29Article 560299

Uhalifu & Adhabu of Wednesday, 29 September 2021

Chanzo: mwananchidigital

Mvua yasimamisha kwa muda kesi ya kina Mbowe

Freeman Aikael Mbowe, Mwenyeketi wa CHADEMA Freeman Aikael Mbowe, Mwenyeketi wa CHADEMA

Kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, imesimama kwa muda kutokana na mvua inayoendelea kunyesha katika maeneo ya Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyoko katika eneo la Shule ya Sheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania), Ubungo jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo imesimama ikiwa ni muda mfupi wakati shahidi wa tatu wa utetezi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi Lilian Kibona kuanza kutoa ushahidi wake leo Jumatano, Septemba 29, 2021.

Kibona ambaye ni mke wa mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adam Kasekwa ameanza kutoa ushahidi huo mbele ya Jaji Mustapha Siyani.

Kutokana na mvua hiyo Jaji Mustapha Siyani anayesikiliza kesi hiyo amelazimika kuahirishwa kwa muda usikilizwaji wa kesi hiyo ili kusubiri mvua iishe baada ya kuondoa usikivu kutokana na kelele za matone ya mvua juu ya paa la ukumbi wa mahakamani hapo.

" Nadhani hatuwezi kuendelea katika hali hii. Naahirisha kwa muda kusubiri mvua ipungue. Siwezi kusema ni kwa muda gani lakini tutaendelea mvua itakapopungua", amesema Jaji Siyani baada ya kushauriana na mawakili wa pande zote.

Kabla ya kufikia uamuzi huo Jaji Siyani aliwauliza kama usikivu unatosha na hasa kwa washtakiwa na mawakili na washtakiwa wakasema kuwa hawasiki.

Kesi ndogo inatokana na maelezo ya Kasekwa ambayo Mawakili wa utetezi waliyapinga yasipokelewe mahakamani kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka wakidai kuwa mshtakiwa huyo hakuyatoa kwa hiyari yake bali aliteswa na kutishiwa na kwamba yalichukuliwa nje ya muda wa kisheria.