Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 09Article 541813

xxxxxxxxxxx of Wednesday, 9 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mwakyembe, Musukuma wamzika ‘Songoro Marine’

ALIYEWAHI kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kisha akawa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika Serikali ya Awamu ya Tano, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku (Musukuma) wameshiriki maziko ya aliyekuwa mmiliki wa kampuni ya Songoro Marine, Saleh Songoro.

Mwakyembe alikuwa naibu waziri wa wizara hiyo katika Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kisha, akawa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Serikali iliyoongozwa na John Magufuli.

Songoro aliyekuwa mmiliki wa kampuni hiyo ya ukarabati na ujenzi wa meli, alifariki dunia hivi karibuni akiwa jijini Mbeya kikazi na mwili wake kusafirishwa na kuzikwa Dar es Salaam juzi. Ameacha mke na watoto wanne.

Katika maziko hayo, Mwakyembe alisema Wizara ya Ujenzi ilibaini uwezo wa Songoro katika kutengeneza meli na kuamua kumwezesha kwa kiasi kikubwa ili kuhakikisha fedha za walipa kodi zinazotumiwa kujenga meli na vivuko zinabakia nchini.

Alisema kuna siku alitembelea ofisi ya Songoro na kisha kukuta uwezo mkubwa aliokuwa nao katika kutengeneza na kukarabati meli huku akiwa ameajiri hadi raia wa kigeni.

Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, serikali pia ilibaini hata baadhi ya kampuni za nje zilizokuwa zikipata zabuni za kutengeneza meli na vivuko, nyingine zilikuwa zikimtumia Songoro kufanya kazi zao na kwa msingi huo, serikali ikaamua kumpa Songoro moja kwa moja kazi za ukarabati na utengenezaji meli.

“Hadi sasa ukienda ofisini kwake utakuta kuna Wazungu wengi wameajiriwa na hii inaonesha kuwa, Watanzania wanaweza kufanya kazi kubwa tena kwa kiwango cha hali ya juu cha ubora,” alisemaMwakyembe.

Akaongeza: “Nchi imempoteza mtu muhimu na aliyekuwa akiwainua Watanzania wengi zaidi hasa kwa kuwafundisha masuala haya ya utengenezaji wa meli na ambaye hakika ameshafanya makubwa kwa taifa hili.”

Kwa upande wake, Mbunge Musukuma alibainisha kuwa, Songoro alikuwa mfano kwa wawekezaji wazawa waliofanikiwa kufanya mambo makubwa kwa taifa.

“Songoro alimudu kufanya kazi za zabuni kubwa na tena kwa ufanisi hususan ujenzi wa vivuko katika Kanda ya Ziwa, Ziwa Nyasa na maeneo mengine nchini,” alisema.

Join our Newsletter