Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 14Article 551494

Uhalifu & Adhabu of Saturday, 14 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mwalimu, mkewe watuhumiwa kuua mtoto waliyemlea

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa.

POLISI mkoani Singida wanamshikilia Mwalimu wa Shule ya Msingi Mang’onyi nwilayai Ikungi, Mathias Marmo (30) na mkewe, Regina Laurent (28) kwa tuhuma za kumuua mtoto mwenye umri wa miaka mitano waliyekuwa wakimlea.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, alisema mjini hapa kuwa, mtoto huyo, Joyce John alifikwa na mauti Agosti 11 mwaka huu saa 1:30 usiku katika Hospitali ya Malkia wa Ulimwengu, Puma alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kipigo cha fimbo kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake.

Amesema kutokana na majeraha yaliyosababisha kifo cha mtoto huyo, wauguzi wa hospitali hiyo walitilia shaka chanzo cha majeraha hayo na kutoa taarifa polisi.

Kamanda Mutabihirwa amesema kuwa baada ya polisi kufanya uchunguzi wao wa awali, walibaini kuwa majeraha yalitokana na kupigwa na walezi wake kwa kutumia vitu vinavyodhaniwa kuwa ni fimbo na kitu butu hali iliyosababisha kifo chake.

Amesema uchunguzi zaidi ulibaini kuwa mtoto huyo alikuwa akipigwa na kufanyiwa ukatili huo mara kwa mara na walezi hao.

Amesema kuwa jeshi hilo linalaani na kukemea vikali vitendo hivyo vya kikatili vinavyofanywa na baadhi ya wazazi au walezi dhidi ya watoto wao.