Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 11Article 546445

Habari Kuu of Sunday, 11 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mwanafunzi aunda mfumo wa kugundua bidhaa bandia

Mwanafunzi aunda mfumo  wa kugundua bidhaa bandia Mwanafunzi aunda mfumo wa kugundua bidhaa bandia

MWANAFUNZI wa shahada ya umahiri katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Jovin John ametengeneza mfumo wa kubaini bidhaa bandia.

Mfumo huo unalenga kuwasaidia wazalishaji, wauzaji na walaji wa bidhaa kuepuka matumizi ya bidhaa bandia na kuimarisha soko la mzalishaji ili apate faida sahihi na kuiwezesha serikali kukusanya mapato.

Akizungumza na HabariLEO katika Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), John alisema alipata wazo hilo baada ya kuona kuna changamoto kwa wazalishaji kulinda bidhaa zao zisitengenezwe bandia na kujua faida halisi wanayopata katika biashara.

“Niligundua wazalishaji hawajui faida halisi wanaoyopata katika mzunguko wa mauzo ya bidhaa zao. Teknolojia hii inawasiadia kujua bidhaa ziko wapi, zimeuzwa ngapi na kama soko limeingiliwa na bidhaa feki. Kupitia mfumo huu anaweza kupanga mipango ya uzalishaji na ubora wa bidhaa zake,” alisema.

Alisema mzalishaji anayetaka kutumia teknolojia hiyo anapaswa kuwa na akaunti maalum katika mfumo na bidhaa zake zinapaswa kuwa na vibali vya mamlaka husika ikiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ndio ziingizwe kwenye mfumo.

“Kuna kifaa maalum kinaitwa TSMS kinatoa mawasiliano sehemu bidhaa zilipo na hii ni teknolojia kutoka nje, kinatumia betri, hiki kinaweza kuwekwa katika maduka makubwa, madogo na sehemu ambako bidhaa husika zipo. Kuna nembo ya mfumo tunaiweka kwenye bidhaa hatua za uzalishaji na popote itakapokuwapo, itaonekana kwenye mfumo,” alisema John.

Akizungumzia teknolojia hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro, Kitivo cha Sayansi na Teknolojia, Idara ya Sayansi za Kompyuta, Dk Morice Daudi alisema Chuo Kikuu cha Mzumbe kinawasaidia vijana kukuza ubunifu wao kitaaluma ili kutoa mchango kwa wananchi na serikali.

Alisema mfumo huo utaisaidia pia serikali kukusanya mapato sahihi ya kodi na kuinua viwango vya ubora wa bidhaa kwa wazalishaji.