Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 21Article 573109

Habari za Afya of Sunday, 21 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Mwarobaini vifo vya uzazi wapatikana

Programu kupunguza vifo vya uzazi yazinduliwa Programu kupunguza vifo vya uzazi yazinduliwa

Taasisi ya Afya Ifakara ikishirikiana na Serikali ya Denmark wamezindua programu ambayo ni nyenzo ya mafunzo kwa njia ya simu na msaada kwa watoa huduma za afya kuhakikisha usalama wa wanawake na watoto wachanga nchini.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikal za Mitaa (OR-TAMISEMI), Grace Magembe amewaambia hayo waandishi wa habari Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa mkutano wa mwaka wa sayansi wa huduma za afya ya uzazi, mtoto, vijana na lishe alisema lengo la programu hiyo, ‘Safe Delivery App’, ni kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Amesema wamekuwa wakijaribu kufikiria ni jinsi gani wanaweza kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi ikizingatiwa nchi ni kubwa na idadi ya watu pia kubwa hivyo ni ngumu kufikia kila mtu.

Magembe amesema itakuwa ngumu na haiwezekani kuwachukua watumishi nchi nzima kuwaweka darasani, lazima kwa kutumia teknolojia, elimu hiyo ya uzazi salama itawafikia watumishi wengi zaidi hususani wale waliokuwa pembezoni ambako ndipo vifo vingi vinapotokea.

Balozi wa Denmark nchini, Matte Spandet amesema wamekuwa wakishirikiana na Tanzania katika mambo mengi yanayohusiana na afya, hivyo anaamini programu hiyo itasaidia kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi. Spandet alisema ana shauku ya kuona kuwa Safe Delivery App inawekwa katika mfumo wa huduma za afya nchini kutoa matokeo endelevu.

Mratibu wa mradi wa Safe Delivery App, Donat Shamba amesema taasisi ya Ifakara ilifanya utafiti wa programu hiyo Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma na kusema imesaidia kwa kiwango kikubwa.

Ameongeza kusema programu ilitumiwa na wakunga, wauguzi kuangalia dawa na huduma gani ili waendelee kutoa huduma baada ya kujifunza. Pia imesaidia kupunguza safari za kumhamisha mgonjwa kutoka hospitali ndogo kumpeleka hospitali za wilaya.